UMASKINI ULIOPITILIZA; Simulizi watu kuuza figo wajikimu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:16 AM Feb 28 2025
Shughuli za uchumi ngazi ya ujasiriamali zinazoendelea mitaani nchini Myanmar, ambako kunatajwa hali kuwa ngumu
PICHA: ZOTE: MTANDAO.
Shughuli za uchumi ngazi ya ujasiriamali zinazoendelea mitaani nchini Myanmar, ambako kunatajwa hali kuwa ngumu

"Nilitaka tu kuwa na nyumba yangu mwenyewe na kulipa madeni yangu, ndiyo sababu niliamua kuuza figo yangu," anasema Zeya, mfanyakazi wa shamba nchini Myanmar.

Bei zilikuwa zimepanda, baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021, hata zikasababisha vita vya wenyewe.

Mtu huyo alikuwa hawezi kumudu gharama ya chakula cha familia yake changa na alikuwa na madeni makubwa.

Akiwa na familia, wakiishi katika nyumba ya mama mkwe wao, katika kijiji chenye nyumba za nyasi kando ya barabara za vumbi. Ni umbali wa saa chache kwa gari kutoka jiji kubwa zaidi nchini humo, Yangon.

Zeya, ambaye si jina lake halisi, kwa ajili ya kulinda utambulisho wake, anasema anawajua watu wa eneo hilo waliouza figo zao, akieleza: "Kwangu walionekana kuwa na afya."

Hapo ndipo akaanza kujiuliza maswali kadhaa na namna yeye anaweza kunufaika, kulingana na hali yake ngumu katika mazingira  hayo.

Huyo ni mmoja wa watu wanane katika eneo hilo walinaojitambulisha kwamba waliuza figo zao kwa kusafiri hadi India.

MIPANGO ILIVYO

Ununuzi au uuzaji wa viungo vya binadamu, unatajwa kuwa kinyume cha sheria nchini Myanmar na India, lakini Zeya anasema alimpata mtu anayempa sifa ya ‘dalali’.

Anasema mtu huyo alipanga vipimo vya kitabibu na wiki chache baadaye, akamwambia kwamba mpokeaji wa figo ambaye ni mwanamke raia  wa Burma, amepatikana na kwamba wote wawili wangeweza kusafiri hadi India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Kisheria, nchini India, ikiwa mtoaji na mpokeaji si ndugu wa karibu, lazima waonyeshe kwamba nia yao ni ya kiutu na kueleza uhusiano wao.

Zeya anasema, dalali huyo alighushi nyaraka, ikiwamo hati ambayo kila kaya nchini Myanmar, lazima iwe nayo, ikiwa na ufafanuzi wanayoeleza maelezo ya wanakaya.

"Dalali aliweka jina langu kwenye sehemu ya familia ya mpokeaji," anaeleza muuzaji figo huyo.

Anasimulia kuwa dalali huyo akafanya ionekane kama alikuwa anatoa figo kwa mtu wa karibu yake, kisha dalali akampeleka kukutana na mpokeaji huko Yangon. 

Huko, anasema mwanamume aliyemtambulisha kama daktari alikamilisha makaratasi zaidi na kumwonya Zeya kwamba, angehitajika kulipa kiasi kikubwa cha pesa, ikiwa angebadilisha mawazo.

Mtu huyo anayetambulishwa kuwa daktari, anasema jukumu lake lilikuwa kuangalia kama mgonjwa anabaki katika hali nzuri ya kufanyiwa upasuaji, si kuthibitisha uhusiano kati ya mtoaji na mpokeaji.

Zeya anasema, akaambiwa kwamba angepokea fedha kati ya milioni 7.5 za Myanmar ni sawa ana Dola za Marekani 2,700 (shilingi 7,074,000).

Anasema alisafiri kwa ndege hadi Kaskazini mwa India kwa ajili ya upasuaji, ambako ulifanyika katika hospitali kubwa.

Upandikizaji wote wa viungo vinavyohusisha raia wa kigeni nchini India, kisheria ni lazima upitishwe na jopo linaloitwa Kamati ya Idhini, ambalo huanzishwa na hospitali au serikali ya eneo husika. 

Zeya anasema, alihojiwa na watu wapatao wanne kupitia mtu aliyekuwa anatafsiri.

"Waliuliza kama nilikuwa ninatoa figo yangu kwa hiari, bila kulazimishwa," anasema.

Anasema alieleza kuwa mpokeaji alikuwa jamaa yake na upasuaji huo ukaruhusiwa.

Zeya anakumbuka madaktari wakampa dawa ya usingizi kabla ya kupoteza fahamu.

"Hakukuwa na matatizo makubwa baada ya upasuaji, isipokuwa sikuweza kutembea bila maumivu," anasema, akiongeza kuwa alikaa hospitalini kwa wiki moja baada ya upasuaji huo.

MZAZI FEKI

Mtoaji mwingine wa figo, Myo Win, pia si jina lake halisi – anasimulia kwamba, alijifanya kuwa ndugu wa mgeni.

"Dalali alinipa kipande cha karatasi na ilibidi nikariri kilichoandikwa," anasema, akiongeza kuwa, akaambiwa aseme kuwa mpokeaji alikuwa ameolewa na mmoja wa jamaa zake.

"Mtu aliyekuwa anashughulikia kesar (tukio) yangu, pia alipiga simu kwa mama yangu, lakini dalali alimpanga ‘mama feki' akapokea simu hiyo," anasema. 

Anaongeza kuwa mtu aliyepokea simu hiyo, akathibitisha kwamba alikuwa akitoa figo yake kwa jamaa kwa ridhaa yake.

Myo Win anasema, aliahidiwa kiasi sawa cha pesa kama Zeya, lakini kiliwasilishwa kama "mchango wa hisani," na ilibidi kumlipa dalali takriban asilimia 10 ya kiasi hicho.

Wanaume hao wawili wanasema walipokea theluthi moja ya pesa hizo, kabla ya upasuaji. Myo Win anasema, hiyo ilikuwa akilini mwake alipokuwa akiingia katika chumba cha upasuaji.

"Nilijiambia kwamba ilibidi nifanye hivyo, kwa sababu tayari nilikuwa nimechukua pesa zao," anaeleza.

Anaongeza kuwa akaichagua njia hiyo, kwa sababu amekuwa akihangaika kulipa madeni na bili za matibabu za mke wake.

UKOSEFU AJIRA

Viwango vya ukosefu wa ajira vimepanda nchini Myanmar tangu mapinduzi yafanyike, inatajwa kuharibu uchumi na kuwafanya wawekezaji wa kigeni kukimbia. 

Mnamo mwaka 2017, robo ya watu wanatajwa kuishi katika umaskini, lakini kufikia mwaka 2023, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi nusu, kulingana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP.

Suala la kukosekana ajira na kuwa katika dimbwi la umaskini ndio chanzo cha wengi kuuza figo zao.

Myo Win anasema, dalali hakumwambia kwamba kuuza figo ni kinyume cha sheria.

“Nisingefanya hivyo kama angeniambia. Ninaogopa kuishia gerezani," anasema, bila kutaja mashirika au watu waliokuwa sehemu ya mpango huu ili kulinda utambulisho na usalama wa waliohojiwa.

Hata hivyo, mwanamume mwingine nchini Myanmar, ambaye akazungumza kwa faragha, anasema alikuwa amesaidia takriban watu 10 kununua au kuuza figo zao kupitia upasuaji nchini India.

Kwa mujibu wa BBC                Â•