Zahanati mpya yenye simulizi ya uzazi wa kujifungulia njiani

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 03:23 PM May 01 2025
Zahanati mpya iliyokuja na mageuzi kijijini Kolagwa, wilayani Mkuranga
Picha: Yasmine Protace
Zahanati mpya iliyokuja na mageuzi kijijini Kolagwa, wilayani Mkuranga

NI ndani ya mtazamo wa dhana ‘usione vyaelea, vimeumbwa’ nchini sasa kuna utitiri wa zahanati na vituo vya afya katika kata mbalimbali nchini.

Hiyo pia, iko katika hospitali ngazi ya wilaya, kupanda ngazi juu kama vile Hospitali za Kanda nchini. 

Kimsingi, ifikapo Julai mwaka huu itatimu miaka 17 ya kupitishwa Sera ya Afya nchini iliyoanza kutekelezwa mwaka 2008.

Hata hivyo, haimaanishi mahitaji yamekamilika kila mahali, bali hatua kubwa imepigwa Tanzania kuwa nchi ya mfano kwa majirani zake.

Tafsiri ya dhana hiyo kama inayoanzia maana ya jina lake kisera ‘afya ya msingi’ (Sera ya Adya ya Msingi) inagusa hata zahanati na kituo cha afya, zikawa karibu na makazi ya watu, uzio wa kata.

Faida mojawapo inagusa umma, ikichangia mwamko wa wajawazito kuhudhuria kliniki kirahisi, hata wanajifungua katika mazingira salama.

Sera nchini inataka kijiji na mtaa kuwa jirani  na zahanati, huku kituo cha afya kwa ngzi ya kata, vivyo hivyo hospitali ya wilaya na kupanda ngazi ya juu kama kabisa, kama vile Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Inafafanuliwa kuwa, umbali wa vituo vya afya unachangia hata wazazi wenye watoto wanaotakiwa kwenda kliniki kupata chanjo na kupimwa uzito.

Umbali unashudiwa kuchangia matukio kama vile watoto kutohudhuria kliniki, kutokana na wazazi au walezi wao kushindwa kumudu gharama za kutoka kijijini hadi penye huduma itakiwayo.

Hapo kunatajwa kama penye vijiji vingine kunakopatikana chanjo au watoto kupimwa, kwenye vituo vya afya vya huko.

MAGEUZI KIJIJINI 

Ndio penye mustakabali wa mfano, hivi karibuni Mwajuma Ally, mkazi wa kijijini Kolagwa wilayani Mkuranga, Pwani akasimulia kuwa ni miaka zaidi ya 20 kijiji chao kimekosa huduma za afya, sasa kikiingia historia mpya ya kuwa na zahanati.

Mwajuma anaeleza walikotoka, kwamba wamekuwa wakitembea kusaka mbadala huduma za afya unoawafikisha kwenye kijiji cha Hoyoyo au Mkuranga, kupata huduma za afya.

Mwajuma anayejitambulisha  mzazi, ananena:"Nina watoto watatu, mtoto wa tatu nimempatia njiani wakati naenda Mkuranga kujifungua." 

Anaongeza kuwa sababu ya kukutwa na mkasa huo wa kujifungua njiani, umetokana na kijiji kutokuwa na huduma za afya, vikiwamo umbali wa kutoka kijijini hadi kijiji kingine.

Hapo anamshukuru diwani wao wa kata ya Tengelea Shaban Manda kwa kukisaidia kijiji hicho kupata zahanati yao.

Abdullah Juma, mkazi wa Kolagwa anasema kuwapo zahanati kijijini hapo, ambayo sasa inakamilishwa,  akiamini itawasaidia kwa huduma za uhakika.

Mkazi huyo anafafanua kwamba, kuwapo zahanati yao kunawasaidia kupunguza gharama za safari kutoka kijijini hapo, hadi kingine wanakofuata matibabu.

"Ukitoka kijijini kwetu kwenda kijiji cha Hoyoyo au Mkuranga, lazima utumie nauli shilingi 10,000 kwa usafiri wa bodaboda. Hiyo ni nauli ya kwenda na kurudi!" anasema.

Hapo ndipo anatoa mtazamo wake kwamba, hatua ya kuanzishwa zahanati hiyo mahali waliko kunawasaidia kupata matibabu kirahisi.

Mkazi huyo anamwelekezea kongole anayemtaja kuwa mbunifu kumfanikishia hatua hiyo, diwani wao anayemtaja kwa jina la Manda, akisema kawasaidia kuhamia katika kupata huduma za afya kwa urahisi na gharama ndogo za usafiri.

Mkazi Abdullah, anafafanua kwamba ni nafuu kwa wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati, watoto wao kupata huduma kama chanjo zote na kuhudhuria kliniki kwa wakati, watoto kupimwa uzito.

UONGOZI WA HALMASHAURI

Diwani wa Kata ya Tengelea, Shaban Manda, anasema kuwa mwaka 2018, ujenzi wa kituo hicho ulianza na kazi hiyo ikasonga kufika upauaji unaogharimu shilingi milioni 50, ukijumuisha nguvu za wanakijiji.

Anaeleza yajayo katika  zahanati hiyo kwa lugha ya ubashiri kwamba “utakuwa mkombozi kwa wanakijiji,” hata baada ya historia  ya mpito wa miaka mingi kutokuwapo zahanati kijijini hapo.

Diwani huyo anaitaja kuwa maendeleo ni makubwa, akiwataka viongozi wenzake wa mahali hapo kujipanga kwa maendeleo hayo na mengineyo.

Katika hatua yake ya ufunguzi, diwani huyo anasema katika hatua ya siku ya ufunguzi, ametoa fedha kwa siku kwa  jamii wenye uhitaji wa matibabu, watibiwe bure.

Hata baada ya hapo, akasema  watatetea matibabu yake kuendelea kutumika kwa kurejea kanuni  husika, kama vile wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano na wazee watapata matibabu bure.

Pia, akaahidi hatua nyingine ya zahanati hiyo kutokuwa na umeme, angeweka kwa gharama zake katika tukio la uzinduzi, mgeni rasmi akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Mohamed Mahundu, akimpongeza diwani kwa kuwajibikia kata yake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kolagwa, Ahmed Kibwana, akafafanua namna walivyokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda vijiji vingine kupata huduma hiyo.

Anakiri simulizi ya namna matukio ya wajawazito kujifungulia njiani, huku wazazi na walezi nao kukawapo  matukio ya kushindwa kuwapeleka kupata chanjo, kutokana na umbali wa vituo vya afya viliko.

Anasema zahanati hiyo iliyofunguliwa kijijini hapo, itatoa huduma za vipimo vyote vidogo na huduma za kujifungua.