Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeshiriki katika Bonanza la Afya la Waajiri (Waajiri Heatlh Bonanza 2025) lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-sehemu ya Mlimani) Novemba 29, 2025.
Bonanza hilo lililobeba kaulimbiu isemayo “Wezesha Uzima, Kuinua Utendaji Kazi” lililenga kukuza afya, tija, na umoja miongoni mwa waajiri na wafanyakazi katika taasisi mbalimbali nchini.
Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambapo sehemu ya watumishi wake walishiriki katika michezo ya Mbio Fupi, Kukimbia na Gunia, Kukimbia na Ndimu, Rede, Kukimbia na glass ya Maji na Kuvuta Kamba wanawake na wanaume.
Katika hatua nyingine kupitia maonesho ambayo yalikuwa sehemu ya bonanza hilo, Meneja wa PSSSF kanda ya Kinondoni, Hajji Khamisi, alisema pamoja na kushiriki michezo hiyo kwa nia ya kuunga mkono afya bora miongoni mwa waajiri na watumishi, pia PSSSF ilitumia fursa hiyo kutoa elimu ya hifadhi ya Jamii kwa kuwaelimisha shughuli zinazotekelezwa na Mfuko na maboresho yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma kupitia PSSSF Kidijitali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED