Fountain Gate yamfungashia virago John Noble kisa magoli ya Yanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:46 AM Apr 22 2025
 Fountain Gate yamfungashia virago John Noble kisa magoli ya Yanga
Picha: Mtandao
Fountain Gate yamfungashia virago John Noble kisa magoli ya Yanga

Uongozi wa Fountain Gate umemsimamisha kipa wao raia wa Nigeria, John Noble, kwa tuhuma za uzembe ulioigharimu timu yao kufungwa mabao 4-0 dhidi ya Yanga.

Noble alicheza dakika 45 za kipindi cha kwanza na kufungwa mabao mawili kabla ya kubadilishwa. Kipa aliyemrithi naye alifungwa mabao mawili.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinasema uongozi haujaridhishwa na makosa mawili aliyoyafanya Noble yaliyochangia kipigo hicho.

“Hatukupendezwa na makosa yake yaliyosababisha timu kutolewa mchezoni kwa uzembe wa mtu mmoja,” chanzo kimoja kilisema.

Kocha wa timu hiyo, Robert Matano, alisema baada ya mechi: 

“Golikipa ametuangusha. Hatutashinda kama tunatoa mabao kwa makosa yetu wenyewe.”

Fountain Gate imefungwa jumla ya mabao 9-0 na Yanga msimu huu, ikiwemo kichapo cha 5-0 kwenye mzunguko wa kwanza, Desemba 29, 2024.