John Bocco atua rasmi JKT Tanzania

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:42 AM Jul 11 2024
 John Bocco.
Picha: Mtandao
John Bocco.

UONGOZI wa klabu ya JKT Tanzania, jana umemtangaza aliyekuwa nahodha wa klabu ya Simba, John Bocco, kuwa mchezaji wao kwa ajili ya Ligi Kuu msimu ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari  na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Masau Bwire, alisema mbali na Boko vile vile wamefanya usajili wa wachezaji  wengine ambao ni Abdurahim Seif Bausi kutoka klabu ya Uhamiaji ya Zanzibar, Charles Martin  (Mtibwa Sugar), Denis Richard  (KMC) na  Karim Mfaume (Biashara United).

Wengine ni Elisha Japhet (Twalipo), Hamis Salum Hamis (KVZ), Kombo Hatibu (Coastal Union) pamoja na Wilson Nanau kutoka klabu ya TMA ya ligi ya Championship.

Pia uongozi huo umemtangaza Jemedary Said kuwa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo pamoja na ile ya wanawake, JKT Queens huku  Hamady Ally akitangazwa kuwa Mkurugenzi wa benchi la ufundi wa timu hizo. 

Alisema kutokana na mabadiliko waliyoyafanya wameteua kamati mbali mbali ikiwamo ile ya mratibu wa JKT Queen itakayoongozwa na Meja Ester Ryoba, huku JKT Tanzania ikiwa chini ya Stanley Joseph. 

Huku Kamati ya Mashindano ikisimamiwa na Luteni Said Lobbe wakati Kamati ya Sheria ikisimamiwa na Kapteni Emmaculata Marunda. 

Vile vile kwa upande wa Idara ya Masoko itaongozwa na Kapteni Spelatus Nyemela na Idara ya Habari na Mawasiliano itaendelea kuwa chini yake (Masau) ambapo mlezi wa timu hizo ni Bregedia Jenerali Hassan Mabena na Mwenyekiti wake atakuwa Geofrey Loyd Mvula. 

Hata hivyo alisema Bodi ya Wakurugenzi itaongozwa na Luteni Kanali Javan Joseph, Luteni Ramadhan Salum pamoja na Meja Mohamed Ayoub Shamsama. 

"Mabadiliko hayo tumeyafanya kwa lengo la kuimarisha kikosi chetu kuelekea mashindano ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara tuweze kushika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi hiyo, alisema Bwire. 

Aliongeza kuwa usajili waliofanya utaleta mapinduzi makubwa katika msimu huo na kuweka wazi malengo yao ni kufanya vema katika michezo yao yote ili wapate nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.