Mrithi wa Chama Simba huyu hapa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:06 AM Jul 02 2024
Jean Charles Ahoua.
Picha:Mtandao
Jean Charles Ahoua.

WAKATI Yanga ikitangaza rasmi kumsajili Mzambia Clatous Chama, baada ya kumaliza mkataba na klabu yake ya zamani, kiungo mshambuliaji anayetajwa kuja kuchukua nafasi yake Simba, Jean Charles Ahoua, anatarajiwa kutua wiki hii nchini kukamilisha usajili.

Habari zilizopatikana ndani ya Klabu ya Simba, na vyanzo mbalimbali vya habari za mchezo Afrika Magharibi, zinasema, Ahoua atasafiri kutoka nchini kwao Ivory Coast kuja nchini kukamilisha usajili wake ambapo kila kitu kimekamilika, kilichobaki ni yeye kutua na kusaini mkataba wa miaka mitatu na kisha kutambulishwa.

Ahoua ndiye mchezaji bora (MVP) kwenye Ligi Kuu nchini Ivory Coast, akiichezea Klabu ya Stella Club d'Adjame ya nchini humo, ambapo amepachika mabao 12 na 'asisti' tisa, hivyo kuhusika katika jumla ya mabao 21 msimu wa 2023/24.

"Huyu ndiye mrithi sahihi wa Chama, anawasili wiki hii, anacheza kiungo mshambuliaji, namba 10, ni mchezaji bora wa msimu wa 2023/24 nchini Ivory Coast, amehusika katika mabao 21, amefunga 12 na asisti tisa, sasa nikwambie tu huyu mchezaji amesajiliwa rasmi kwenda kuchukua mikoba ya Chama, huyu ndiye atakayeuzika ufalme wake.

"Viongozi wameachana na Chama kwa sababu kwanza umri umekwenda halafu amekuwa msumbufu, na kwa kiasi kikubwa kwa kipindi cha karibuni nidhamu yake haikuwa nzuri," alisema mtoa taarifa wetu ndani ya klabu hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri miaka 22, alizaliwa Februari 10, 2002 nchini humo, na alianza soka la ushindani, mwaka 2020 alipocheza kwenye Klabu ya  LYS Sassandra na mwaka huo huo, akahamia Sewe FC, ambayo alikipiga nayo hadi 2022, alipojiunga na Stella Club d'Adjame kabla ya kuwavutia mabosi wa Simba ambao baadhi yao walisafiri mpaka nchini humo kutaka huduma yake.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema kwa sasa wanaendelea na usajili na mpaka watakapomaliza ndipo watakapoanza kutangaza mmoja baada ya mwingine.

Amekiri kuwa baadhi ya wachezaji wataingia wiki hii, lakini tayari kuna wachezaji saba wametua kwa ajili ya kumalizana na uongozi.

"Tuna wachezaji wapya saba wa kigeni wapo hapa hapa Tanzania kwa ajili ya usajili, bahati nzuri si watu wengi wanaowafahamu, lakini pia wapo chini ya ulinzi mkali, napenda kuwaambia wanachama na mashabiki wa Simba wasione kimya wakadhani hakuna kinachofanyika. 

"Wakati haya majembe saba yapo Dar, baadhi ya viongozi wetu wamegawana majukumu, mwingine Zambia, yupo aliyekwenda Ivory Coast, kuna anayesafiri kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, mmoja Maylasia, kote huko kwenda kumalizana na wachezaji," alisema Ahmed.

Alisema kwa mara ya kwanza baada ya misimu mingi Simba itakuwa na wachezaji wengi wapya kwenye kikosi chake na hii inafanywa makusudi na uongozi ili kutengeneza timu mpya itakayorudisha heshima ya klabu hiyo.

"Tunafanya ukarabati mkubwa, timu hii lazima tuijenge upya, watu wamechoka, wanataka furaha, wanataka makombe, hawataki kuendelea kuyaona ya zamani, wanataka kuyaona mapya, huwezi kuyapata kama hujatengeneza timu bora," alibainisha Meneja Habari huyo.