Pacome, Mpanzu vinara wa 'asisti'

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:01 PM Nov 18 2025
news
Picha Mtandao
Winga wa Simba, Elie Mpanzu.

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, winga wa Simba, Elie Mpanzu na beki wa kati wa Dodoma Jiji, Abdi Banda, wanaongoza kwa kutoa pasi za mwisho za mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara hadi kufikia sasa.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Takwimu cha Dawati la Michezo Nipashe, wachezaji hao wametoa 'asisti' mbili kila mmoja ambazo zilizaa mabao.

Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa Mpanzu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ana 'asisti' mbili akiwa amecheza dakika chache zaidi kuliko wenzake.

Akicheza dakika 165, Mpanzu alitoa pasi ya bao Septemba 25, mwaka huu, alipotoa krosi ya bao la pili lililofungwa na Jonathan Sowah, Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kabla hajafanya tena hivyo, Novemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, alipopiga krosi iliyomkuta Wilson Nangu aliyejitwisha mpira ukajaa wavuni, Simba ikishinda mabao 2-1, dhidi ya JKT Tanzania.

Banda, ambaye amerejea nchini baada ya kucheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini, ndiye mtoa 'asisti' aliyecheza dakika nyingi 540, kuliko wengine.

Kwa upande wa Pacome, aliyecheza kwa dakika 195 raia wa Ivory Coast, alitoa pasi ya mwisho Septemba 24, kwa Mudathir Yahaya, aliyefunga bao la tatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, nyingine ikiwa ni Novemba 9, mwaka huu, alipotoa pasi ya bao la kwanza kwa Maxi Nzengeli, Yanga ikiicharaza KMC mabao 4-1, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Msimu uliopita, Pacome alishika nafasi ya pili kwa 'asisti' ambapo alitoa pasi 10 akiwa na timu yake ya Yanga, ambapo kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum, ndiye aliyemaliza ligi akiwa kinara wa 'asisti' akifanya hivyo mara 13.

Mpanzu alimaliza na 'asisti' sita, hivyo msimu huu kuonekana mapema kwenye kinyang'anyiro cha kuwania mshindi wa kutoa pasi za mwisho.

Wakati wachezaji wa JKT Tanzania, Paul Peter na Salehe Karabaka wakiongoza kwa ufungaji mabao, kila mmoja akifunga matatu, straika Peter, pamoja na kufunga ametoa 'pasi moja ya bao.

Hata hivyo, straika huyo amecheza dakika nyingi kuliko mwenzake Karabaka, ambaye amefunga mabao matatu, lakini haa 'asisti' yoyote mpaka sasa.

Peter ambaye pia anaichezea Timu ya Taifa, Taifa Stars, amecheza dakika 527, winga Karabaka, anayeichezea JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba, akicheza kwa dakika 361.

Wachezaji waliofunga mabao mawili kwenye Ligi Kuu na 'asisti' ni Mateo Antony na Vitalisy Mayanga, wote wa Mbeya City, Maxi Nzengeli wa Yanga, Fei Toto wa Azam, na Athumani Masumbuko 'Makambo' wa Coastal Union na Vitalisy Mayanga wote wakiwa na 'asisti' moja kila mmoja.

Waliofunga mabao mawili mpaka sasa bila 'asisti' ni Andy Boyeli wa Yanga, Febrice Ngoy wa Namungo na Rushine de Reuck wa Simba.