NYOTA wa Yanga, Pacome Zouzoua, amesema yeye na wachezaji wenzake wemetua Algeria kwa lengo la kupambana na kuipigania timu hiyo kupata ushindi kwenye mchezo wao wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya JS Kabylie.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa Ijumaa jijini Alger ambapo Yanga itaingia uwanjani ikiwa imetoka kupata ushindi kwenye mchezo wake wa kwanza nyumbani dhidi ya AS FAR ya Morocco mwishoni mwa wiki iliyopita.
Pacome, akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili nchini humo, alisema lengo lao walililokubaliana kama timu ni kuhakikisha wanapata ushindi na kuendelea kuipambania timu hiyo.
Alisema benchi la ufundi la timu hiyo tayari limefanya kazi yake kwa kuwapa mbinu ya kucheza ugenini ili kupata matokeo mazuri.
"Tunafahamu hautakuwa mchezo mwepesi, lakini tumekubaliana tupambane kuanzia dakika ya kwanza mpaka filimbi ya mwisho..., tumekuja huku kuipambania Yanga," alisema Pacome.
Juzi akizungumza kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kuanza safari, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema wataingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kushambulia muda wote ili kupata ushindi.
Kocha huyo alisema hawana sababu ya kucheza kwa kujilinda na kwamba, watahakikisha wanamiliki mpira na kutengeneza mashambulizi kwa wingi.
JS Kabylie itaikaribisha Yanga huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa kwanza wa kundi hilo dhidi ya Al Ahly ambapo walikubali kipigo cha mabao 4-1 na kujikuta wakiburuza mkia nyumba ya AS Far.
Kwa matokeo ya michezo ya kwanza, Al Ahly wanaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga wakiwa na manne na kuruhusu bao moja, Yanga wanashika nafasi ya pili nao wakiwa na pointi tatu na bao moja kutokana na ushindi wa 1-0 walioupata wiki iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan mjini Zanzibar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED