KUMEKUWA na usiri mkubwa kwenye kambi za wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga kuelekea kwenye michezo yao ya kimataifa.
Makocha wa timu hizo kwa sasa wamekuwa kimya kabisa bila kuongea chochote, wakiendelea na mipango yao kuelekea kwenye michezo hiyo, huku Maofisa Habari nao wakikataa kuzungumzia mambo mbalimbali ya kiufundi ya makocha wao, badala yake wakihamasisha mashabiki kwenda uwanjani.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, itacheza dhidi ya AS FAR ya Morocco, Jumamosi ijayo, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, huku kukiwa na usiri mkubwa juu ya mipango ya makocha wa timu hiyo kuelekea mchezo huo, Pedro Goncalves na msaidizi wake, Patrick Mabedi.
Makocha hao kwa sasa wamekuwa kimya kuelezea mikakati yao, huku Ofisa Habari, Ali Kamwe, akibainisha mambo machache, ikiwamo urejeo mazoezini wa wachezaji Ibrahim Hamad 'Bacca' na Edmund John.
"Walimu ni wapya kwa sasa kazi yao kubwa ni kukiandaa kikosi tu siyo kuzungumza, pia wanahitaji sapoti ya viongozi, ndiyo maana kwa sasa viongozi wetu wamekuwa wakihudhuria mazoezi kuelekea kwenye mchezo huo muhimu.
Kifupi kwetu ni mchezo muhimu na tunahitaji kushinda, mikakati yote inafanywa ili kuhakikisha tunapata ushindi, kikosi kinatarajiwa kuondoka Jumanne au Jumatano kuelekea Zanzibar kwa boti, wapinzani wetu bado hawajasema wanaingia lini, lakini sisi tunajua janja ya timu za Afrika Kaskazini, wanaweza kuwaambia wanakuja leo, wakaja kesho, au wakawaficha muda wa kuwasili, haijalishi, tutakutana uwanjani," alisema Kamwe.
Kwa upande wa Simba, Meneja Mkuu, Dimitar Pantev na Msaidizi wake, Selemani Matola, nao mpaka sasa hawajaongea chochote kuelekea kwenye mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Petro de Luanda ya Angola.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema ukimya wao ni kwa sababu wako kazini kukiandaa kikosi kwa ajili ya mchezo huo, ambapo yote yanayofanyika huko ni siri ya kambi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika mkutano uliofanyika Soko la Stereo, Temeke, Ahmed alisema maandalizi yanaendelea vizuri licha ya kukosekana kwa wachezaji wawili muhimu.
Alisema mlinda mlango Moussa Camara, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa goti leo nchini Morocco ambapo atakaa nje kwa wiki nane hadi 10, huku beki wao, Abdulrazack Hamza akiondoka wiki hii kuelekea nchini humo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo zaidi.
Kwa upande mwingine, Ahmed aliwatoa hofu mashabiki kuhusu kiungo wao, Mohammed Bajaber, akibainisha kuwa amepona kwa asilimia 100 na tayari ameanza kufanya mazoezi na wenzake takribani wiki mbili tangu apone na juzi alicheza katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya JKT Tanzania.
"Maandalizi yanaendelea vizuri. Hivi karibuni tulicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT Tanzania na kushinda mabao 6-0. Ushindi haukuwa lengo kuu, bali Meneja wetu Mkuu Dimitar Pantev alitengeza mipango ya kumwua mpinzani wetu," alisema Ally.
Alibainisha kuwa wapinzani wao wanatarajiwa kuwasili nchini kesho na waamuzi watakaochezesha mchezo huo wanatoka Congo Brazzaville.
Katika hatua nyingine, Simba imetangaza ratiba ya hamasa kuelekea mchezo huo, ambapo uzinduzi utafanyika kesho katika tawi la Simba Zingiziwa, Chanika. Novemba 20 hamasa itaendelea Goba, huku Novemba 21 wakitoa msaada katika kituo cha watoto yatima Temeke na Novemba 22, mwaka huu watakamilisha kampeni hiyo maeneo ya Vikindu.
Aidha, viingilio vya mchezo huo kwa Tanzanite Sh. 250,000, Platinum Sh. 150,000, VIP A Sh. 30,000, VIP B Sh. 20,000 na mzunguko Sh. 5,000 ambapo tiketi zilianza kuuzwa hapo jana.
Aidha, alisema uzinduzi wa jezi za mchezo huo unatarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii jijini Dar es Salaam.
Ahmed alisema mechi ya Jumapili itakuwa ngumu, hivyo kuwataka mashabiki kujaza uwanja kwa ajili ya kuwatia moyo wachezaji kama ilivyo kawaida yao.
"Mara zote Simba nguvu yao imekuwa ni mashabiki, mara zote walipokuja uwanjani na kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa hata katika michezo migumu, ilipata ushindi kwenye matokeo ambayo hayakutarajiwa.
"Hatujazoea na hatujawahi kuishia hatua za makundi tangu tuanze kutawala soka la Tanzania," alisema.
Hata hivyo, alisema hawaichukulii poa timu hiyo hata kidogo, na kwamba taarifa walizonazo ni kwamba ni moja kati ya timu bora nchini Angola.
"Mwaka huu vilevile tumejipanga kuvuka, tunahitaji tufanye kazi kweli kweli. Haitokuwa mechi nyepesi, ili kuvuka ni lazima tuifunge Petro de Luanda," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED