SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa wito kwa mikoa kuhakikisha inaratibu vizuri Ligi za Mikoa kwa kuhakikisha vijana wengi wanapata nafasi ya kucheza kwa ajili ya maendeleo ya soka nchini.
Hayo yalisemwa juzi jioni na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Oscar Mirambo, wakati alipokuwa anafungua rasmi Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), ufunguzi ambao ulifanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi.
Katika ufunguzi huo, timu ya Dream Soccer City iliichapa Bara FC mabao 2-1, mchezo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.
"Ninatoa wito kwa mikoa mingine kuratibu timu zao za mikoa ziwe zinacheza vizuri Ligi ya Mkoa kama unavyofanya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa sababu kijana anayecheza Ligi hii akipata timu kubwa anafanya vizuri kutokana na uzoefu aliokuwa nao," alisema Mirambo.
Katibu huyo aliupongeza uongozi wa DRFA kutokana na juhudi kubwa unazozifanya kuhakikisha ligi hiyo inafanyika kwa weledi mkubwa.
"Kwa upande wa Mwenyekiti wa DRFA, Lameck Nyambaya, alisema ligi hiyo inashirikisha timu 28 kutoka wilaya za mkoa huo ambapo kutakuwa na makundi tofauti tofauti, na kudai kila kundi litagawanywa timu mbilimbili.
"Ligi ya msimu huu itakuwa na ushindani kutokana na aina ya timu zilizopo, ambapo michezo itakuwa inachezwa kwenye viwanja mbalimbali vilivyopo ndani ya mkoa wetu wa Dar es Salaam," alisema Nyambaya.
Alisema msimu huu wamefanya maboresho makubwa kwa upande wa zawadi na kwamba mshindi wa kwanza ataibuka na shilingi milioni 10.
Nyambaya alisema kwa sasa wamehakikisha wachezaji wote wanaoshiriki ligi hiyo ni wale wenye vigezo vya umri na kuweka wazi atakayebainika amedanganya umri atafukuzwa na timu yake kufungiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED