Afrika yatakiwa kutumia fursa ya zao la kahawa kwa tija

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:21 PM Feb 26 2025
Afrika yatakiwa kutumia fursa ya zao la kahawa kwa tija.
Picha:Mpigapicha Wetu
Afrika yatakiwa kutumia fursa ya zao la kahawa kwa tija.

Afrika imetakiwa kutumia vizuri fursa zinazotokana na zao la kahawa, ambalo linazalishwa na wakulima katika maeneo mbalimbali ya bara hilo, ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi na kilimo hicho.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mwandamizi wa Mashariki na Kusini mwa Afrika wa taasisi ya Rainforest Alliance, Julius Ng’ang’a, wakati wa kongamano la maonyesho ya Wiki ya Kahawa Afrika lililowakutanisha wakulima na wadau wa kahawa kutoka ndani na nje ya nchi.

Ng’ang’a amesema kuwa ingawa kahawa inalimiwa na mamilioni ya wakulima barani Afrika, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama umasikini na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, amesema taasisi yake inaendelea kusaidia wakulima kuboresha uzalishaji na maslahi yao kwa kuwapa mbinu bora za kilimo.

“Mbali na kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji, tunawaunganisha pia na masoko mazuri. Hata hivyo, ili kuwalinda dhidi ya changamoto kama mabadiliko ya hali ya hewa, tunapaswa kuwapa mafunzo ya jinsi ya kulima kwa njia endelevu,” amesema Ng’ang’a.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo inawahamasisha wakulima kupanda mazao mengine kama maparachichi kwenye mashamba yao ya kahawa ili kuwa na vyanzo mbadala vya kipato endapo bei ya kahawa itashuka sokoni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kahawa kilichopo Bukoba, Amir Hamza, amesema kongamano hilo limekuwa na manufaa kwa wakulima na wadau wa kahawa, hasa katika kuwapa elimu juu ya athari za matumizi ya dawa zisizofaa katika zao hilo.

1

“Ni vigumu kwa taasisi moja kushughulikia sekta nzima ya kahawa kwa sababu inajumuisha hatua nyingi kama uvunaji, ununuzi, usafirishaji, na masoko. Ushirikiano na mshikamano kati ya wadau ni muhimu,” amesema Hamza.

Amezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima wa kahawa kuwa ni gharama kubwa za vifaa vya kuongeza thamani ya zao hilo na ukosefu wa elimu ya usindikaji.

“Kuongeza thamani kwa zao la kahawa ni muhimu ili mkulima aweze kuuza kwa bei nzuri na kuepuka madhara ya kushuka kwa bei ya soko la dunia. Njia mojawapo ni kuhamasisha Watanzania kupenda kunywa kahawa,” ameongeza.

Kuhusu changamoto za biashara ya kimataifa, Hamza amesema kikwazo kikubwa ni gharama na urasimu wa usafirishaji wa kahawa kutoka nchi moja kwenda nyingine, pamoja na baadhi ya nchi kuwa na sheria zinazozuia uingizaji wa kahawa kutoka nje.

“Zamani tulitumia redio kutangaza kahawa yetu, lakini sasa tunalazimika kutumia mitandao ya kijamii ili kuwafikia wateja wengi zaidi,” amesema Hamza.

Ameeleza kuwa mikakati iliyopo sasa ni kuongeza thamani ya kahawa kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kwa bei nafuu, hatua inayolenga kuwavutia vijana wengi ambao hupendelea vinywaji vyenye ladha laini badala ya kahawa chungu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Prof. Aurelia Kamuzora, amesema serikali itaendelea kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti ili kuhakikisha uzalishaji wa kahawa bora.

“Mabadiliko ya tabianchi yameleta athari kubwa, mfano hapa Dar es Salaam joto limeongezeka kwa kiasi kikubwa. Ugeni huu umetuletea hoja ya upandaji miti kama sehemu muhimu ya uzalishaji endelevu wa kahawa,” amesema Prof. Kamuzora.

Ameeleza kuwa serikali inaendelea kupinga ukataji miti kiholela na kuhamasisha matumizi ya nishati safi, kama inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.