Baraza la Madiwani Mkuranga lapitisha taarifa za miradi ya maendeleo

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 01:26 PM Apr 29 2025
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Salum Mwela.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Salum Mwela.

Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani limepitisha taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha.

Akizungumza katika kikao cha baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Salum Mwela, alisema madiwani wamepitisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2024/2025, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 14 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, zikigawanywa katika robo nne kupitia mapato ya ndani.

Aidha, Mwela alisema kuwa pamoja na ajenda ya miradi ya maendeleo, kikao hicho pia kilitumika kutoa elimu kwa madiwani kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote.

"Tumepata elimu, hii elimu tutaitumia kuwafikishia wananchi ili wajue umuhimu wa bima ya afya kwa wote," alisema.

Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mwela alisema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kipenzi cha watu wa Mkoa wa Pwani, wakiwemo wananchi wa Mkuranga, kutokana na namna serikali yake inavyowaletea maendeleo kupitia miradi mbalimbali mikubwa.

Alisema kupitia serikali hiyo, Mkuranga imenufaika na mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano unaotekelezwa eneo la Mkwalia, ambao unahudumia wakazi wa Kata ya Mkuranga pamoja na vijiji vya jirani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Salum Mwela.
Vilevile, alisema Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga imeboreshwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 900 kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Mwela alibainisha kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa kupata zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya ufundi katika Kata ya Mkamba, Kijiji cha Kizapara.

Aliongeza kuwa pia wamefanikiwa kupata mradi wa maji kwa vijiji saba katika halmashauri hiyo, sambamba na uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari, akisema:

"Pongezi kubwa zimfikie Rais Samia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Mkuranga. Shukurani zetu kwa Mama Samia tutazionyesha Oktoba mwaka huu katika Uchaguzi Mkuu," alisema Mwela.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Abdallah Ulega, kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha 2015 hadi 2025.

Alisema mbunge huyo amefanikisha uboreshaji wa barabara nane kutoka TARURA hadi TANROAD, zikiwemo barabara za Vikindu, Marogoro, Sangatini, Kiguza, Mwanaderatu mpaka Kitonga, Kimanzichana, Mkuluwili hadi Msanga, na Mkuranga-Tengelea-Dondwe hadMvuti.Mvuti.