Bodi ya EWURA yatembelea Bomba la Mafuta TAZAMA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:49 PM Mar 23 2025
Bodi ya EWURA  yatembelea Bomba la Mafuta TAZAMA
Picha: Mpigapicha Wetu
Bodi ya EWURA yatembelea Bomba la Mafuta TAZAMA

Mwenyekiti wa Bodi ya ya Wakurugenzi ya EWURA, Prof. Mark Mwandosya leo 23 Machi 2025, ameongoza wajumbe wa Bodi hiyo na Menejimenti kwenye ziara ya kutembelea Bomba la Mafuta la TAZAMA linaloanzia Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola, Zambia. Ziara hiyo ilianza Machi 21, 2025.

5Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati ya Bodi hiyo, Mha. Ngosi Mwihava amesema lengo la ziara hiyo ni kutizama utekelezaji wa masuala ya kiuchumi, kimiundombinu na uendeshaji wa bomba la TAZAMA.

“Moja ya jukumu la EWURA katika sekta ya petroli ni kudhibiti miundombinu ya usafirishaji wa mafuta na gesi asilia, hivyo ziara hii ni mahsusi kwa ajili ya kutembelea miundombinu ya bomba, kuona changamoto zilizopo na kuangalia namna tunavyoweza kusaidia utatuzi wa changamoto hizo ili kuendelea kuboresha huduma za usafirishaji wa mafuta kupitia bomba hili” amesema.



Mha. Mwihava ameongeza kuwa,  ziara hiyo ni fursa kwa Bodi ya EWURA na ya Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya upangaji wa bei, mikakati ya uhifadhi wa mafuta ya akiba na kujengea wataalamu uwezo.

Ujumbe huo pia, umetembelea kituo cha Chilolwa cha kuangalia usalama wa bomba la mafuta, kituo cha kusukuma mafuta kilichopo Chinsali na ghala la kuhifadhia mafuta lililopo Mpika.


Maeneo mengine yaliyotembelewa ni kituo cha Kilonje cha kusukuma mafuta, kituo cha Mulilima cha kutuma na kupokelea kifaa cha kufanya usafi wa bomba, na kituo cha kupokelea mafuta cha Bwana Mkubwa  ambacho kiko Ndola. 

Ujumbe huo pia utakutana na  uongozi la Bomba la TAZAMA, Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) pamoja na Baraza la Udhibiti wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Zambia (NWASCO) ili kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kisekta.

3