BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kuwa noti za fedha ya kitanzania zina muda wa ‘kuishi’ kama binadamu, hivyo ni lazima zituzwe na kuheshimiwa kwa kuwa ni tunu ya Taifa kama zilivyo nyingine.
Hayo yamesemwa Februari 26, 2025 na Ofisa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu, Itika Mwakisambwe, wakati akiwasilisha mada ya Historia ya Fedha za Tanzania, alama za usalama na utunzaji wa fedha hizo kwa waandishi wa habari waandamizi wanaohudhuria semina mkoani Mtwara.
Amesema kama ambavyo binadamu unaambiwa ule hiki, ufanye hivi ili ujitunze na kuishi muda mrefu, basi na fedha yetu nayo inapaswa kutunzwa kwa kuhifadhiwa vizuri, isichafuke kwa kuwa ni tunu yetu kama nchi.
“Kama tunavyosikia Prof, Janabi anashauri kula hiki na kile ili uwe salama kiafya, basi na noti zinapaswa kutunzwa kuwa zina muda wake wa kuishi. Kwa BoT tunakadiria muda wa kuishi wa noti ni miaka miwili.Hatutakiwi kutoboa noti zetu, tunazipunguzia muda wake wa kuishi, fedha ina ishi kama binadamu inatakiwa kutunzwa.Mtu anapewa chenji ikiwa imekunjwa naye anaweka hivyo hivyo, lazima unyooshe na utunze fedha kama inavyotakiwa ili idumu,”amesema.
Itika ametolea mfano kwenye nyumba za ibada ambako mtu anatoa sadaka kwa kukunja noti lakini inawezekana kuweka utaratibu mzuri zikawekwa kwenye bahasha au zitolewe kidijitali ili zisiharibike.
“Kwenye kutoa sadaka tunaambiwa utoacho hata mkono wako mwingine usijue, unakuta mtu anakunja noti hii inaharibu fedha yetu, ni bora iwekwe kwenye bahasha au utaratibu wa dijitali.Wakinadada wana wallet zinazokunja fedha zaidi ya mara moja, bora wanaume zao zinakunja mara moja fedha inakuwa salama, tuhakikishe tunaitunza fedha yetu ili thamani yake izidi kuwepo na kuipenda tunu yetu.”
“Kuna wanaoandika kwenye noti ili kuona kama itamrudia kwenye mzunguko, kufanya hivyo ni kuhartibu fedha. Kuna waasibu hupenda kuzibana kwa pini fedha jambo ambalo si sahihi, fedha ya aina hii ikifika BoT tunaiharibu, ni hasara kwa nchi.
“Ni nia ya BoT kuhakikisha fedha iliyopo kwenye mzunguko ni safi, inaporudi wanaziondoa kwenye mzunguko zinaharibiwa,”amesema.
“Maisha ya noti yanatofautiana kutokana na namna zinazotumiwa, ila inatarajiwa ikae kwa miaka miwili ili kutambua alama zote za utambuzi,”amefafanua.
Alipoulizwa ni kwanini Tanzania hatutumii senti kwenye manunuzi, amefafanua zaidi kuwa katika matumizi ya fedha huwezi kuona manunuzi ya senti moja nchini kwa kuwa ndio tabia ya fedha yetu kutokana na uchumi wetu.
Itika amefafanua kuwa noti feki nyingi ni ambazo wanazitoa nakala ndio maana wanasisitiza wananchi kuzingatia alama za utambuzi wa fedha zilizopo halali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED