Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya nishati imepiga hatua kubwa, huku nchi ikiwa na uzalishaji wa umeme wa ziada unaozidi mahitaji ya Watanzania.
Dk. Biteko aliyasema hayo Machi 23, 2025, jijini Arusha, wakati wa Kikao cha Baraza Kuu la Wazazi Taifa, ambapo alieleza ongezeko la mahitaji ya umeme nchini na uwekezaji mkubwa uliotekelezwa katika sekta hiyo.
"Rais Samia amefanya kazi kubwa katika sekta ya nishati nchini, na hivi karibuni tulikuwa nchini Barbados kueleza mafanikio yetu katika sekta hii kwa kuwa ameweka jitihada kubwa sana katika kukuza nishati," alisema Dk. Biteko.
Aliongeza kuwa sekta ya nishati ni nguzo muhimu kwa uchumi wa taifa, akieleza kuwa viwanda vinahitaji asilimia 40 ya umeme wote unaozalishwa, huku sekta ya madini ikihitaji asilimia 30.
Dk. Biteko alitoa takwimu zinazoonyesha ongezeko la mahitaji ya juu ya umeme nchini katika miaka ya hivi karibuni:
Alisema ongezeko hilo la mahitaji halingewezekana bila uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya nishati.
Aidha, alitangaza kuwa Machi 22, 2025, mashine ya tisa ya mtambo wa kuzalisha umeme katika Bwawa la Julius Nyerere imekabidhiwa na kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, hatua inayoongeza upatikanaji wa umeme wa kutosha kwa Watanzania.
"Kwa sasa, Bwawa la Julius Nyerere pekee linaweza kutosheleza mahitaji ya nchi, na hata mitambo ya kuzalisha umeme ya Songas inaweza kusitisha uzalishaji wake bila kuathiri upatikanaji wa umeme," alisema Dk. Biteko.
Katika kikao hicho, Wizara ya Nishati kupitia taasisi zake TPDC, REA na TANESCO, ilitoa semina kuhusu Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 na umuhimu wa matumizi sahihi ya nishati safi ya umeme.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Ngeleja Mugejwa, alieleza kuwa matumizi ya nishati safi yana faida kubwa, hususan kwa watoto wa kike, kwa kuwa yanawapunguzia muda wa kuandaa na kupika chakula, hivyo kuwawezesha kupata muda mwingi wa kujisomea.
Aidha, Dk. Biteko alitoa wito kwa Watanzania kuzingatia matumizi bora ya umeme na kuacha tabia zinazosababisha upotevu wa nishati, akisema kuwa utafiti wa Wakala wa Nishati wa Kimataifa (International Energy Agency) umebaini kuwa asilimia 30 ya umeme unapotea kutokana na matumizi mabaya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED