MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imezitaka kampuni za gesi kuongeza idadi ya mawakala wa usambazaji, ili kuepusha watu kununua gesi kwa wauzaji wasio rasmi.
Wito huo umetolewa leo, Aprili 24, 2025 na Meneja wa Ewura, Kanda ya Mashariki, Mhandisi Nyirabu Musira, wakati akifungua semina kwa wasambazaji wa gesi za kupikia (LPG), yenye lengo la kuhakikisha LPG unafanyika kwa njia zilizo halali na salama kwa watu na mazingira.
Amesema uchakachuaji wa gesi ya kupikia ni changamoto ambayo imekuwa ikiongezeka siku za hivi karibuni, wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia mitungi kujaza mitungi midogo kwa kiwango hafifu.
"Zipo changamoto kadhaa kwenye biashara hii ya LPG, lakini changamoto ambayo imekuwa ikiongezeka sana kwa siku za hivi karibuni ni ujazaji haramu wa mitungi ya gesi.
"Niwaonye wafanyabiashara kuacha tabia hii kwani ni kinyume cha taratibu na sheria, tunaendelea na ufuatialiaji, watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao," amesema.
Aidha ametoa wito kwa mawakala wa LPG, kuhakikisha wanakuwa na leseni hai za EWURA na wanafanya biashara, kwa kufuata masharti ya leseni.
"Hili ni ongezeko la asilimia 38 ukilinganisha na kiasi cha Tani 293,167 zilizoingizwa nchini mwaka 2022/23. Kulingana na rekodi zetu ongezeko hili ndilo kubwa kwa takribani miaka mitano iliyopita," amesema Mhandisi Musira.
Hata hivyo amesema kuwa, EWURA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhamasisha matumizi sahihi ya gesi, ili kuepuka majanga ya moto yatokanayo na gesi za majumbani.
Ahmed Sharifu, ambaye ni wakala wa gesi, wilayani Temeke, amesema semina hizo zinawasaidia katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku.
"Tunawashukuru Ewura kwani semina hizi zinatupa maono ya mbele na kujua matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yetu na hii inaonesha kwamba kazi kubwa ya Ewura ni kutuelimisha katika usalama na kujua utaratibu wa kupata leseni," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED