Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea na kampeni yake ya kuwafikia wafanyabiashara na wananchi waliojiajiri kwa kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na mpango wa Hifadhi Scheme. Katika zoezi hilo, timu ya NSSF imefanya uhamasishaji eneo la Kariakoo Sokoni, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha kundi kubwa la wananchi linafaidika na hifadhi ya jamii.
Akizungumza wakati wa kampeni hiyo, maafisa wa NSSF wameeleza kuwa mpango wa Hifadhi Scheme unawalenga wananchi waliopo kwenye sekta zisizo rasmi kama vile wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, waendesha bodaboda na bajaji, pamoja na wafanyabiashara wadogo kama machinga, mama/baba lishe, wauza mkaa, na wasusi.
"Ni rahisi sana kujiunga na NSSF. Mwananchi anaweza kuchangia kwa kupiga 15200# kisha kufuata maelekezo. Hii ni fursa ya kipekee kwa wale waliojiajiri kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa mafao yao ya uzeeni na kinga dhidi ya majanga mbalimbali," amesema mmoja wa maafisa wa NSSF.
NSSF imesisitiza kuwa mpango wa Hifadhi Scheme unatoa mafao mbalimbali, ikiwemo pensheni ya uzeeni, mafao ya matibabu, ulemavu, na manufaa mengine yanayolinda ustawi wa wanachama wake.
Wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo ili kuhakikisha wanajenga msingi imara wa maisha yao ya baadaye kwa kuwa na uhakika wa mafao yao pindi wanapohitaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED