Serikali yatumia shilingi bil. 94.5 kukamilisha ujenzi wa Vyuo 33 vya ufundi

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 04:42 PM Mar 03 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore.
Picha: Paul Mabeja
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore.

Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 94.5 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo 33 vya ufundi stadi, ambapo 29 kati ya hivyo ni vya wilaya na vinne ni vya mkoa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore, alibainisha hayo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kasore alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, serikali ilitenga shilingi bilioni 103 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vipya 64 vya wilaya pamoja na chuo kimoja cha mkoa wa Songwe. Vyuo hivyo vitasaidia kuongeza fursa za elimu ya ufundi kwa wanafunzi 89,700.

“Kwa sasa VETA ina jumla ya vyuo 80, na ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025, vyuo vipya vinavyojengwa vitakapokamilika, idadi hiyo itaongezeka hadi 145. Hii itakuwa hatua kubwa katika kuhakikisha vijana wa Kitanzania na hata watu wazima wanaoelekea kustaafu wanapata mafunzo ya ufundi yatakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa,” alisema Kasore.

Akizungumzia juhudi za serikali katika kuboresha elimu ya ufundi stadi, Kasore alieleza kuwa VETA imeendelea kupanua miundombinu yake kwa kuongeza majengo mapya na kukarabati yale ya zamani ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia.

"Ili kuhakikisha ubora wa mafunzo na kuongeza fursa za udahili, serikali imetoa shilingi bilioni 14.2 kwa kipindi cha miaka minne kwa ajili ya upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya vyuo vya VETA," aliongeza.

Hatua hizi ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha elimu ya ufundi stadi nchini, ili kuwapa vijana ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita tarehe 3 Machi, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.