BAADA ya miaka 40 ya tabu ya kujisaidia kwenye migomba, nyuma ya mapagare na makazi ya watu, kutokana na kukosekana kwa huduma ya choo katika Soko la Walaji la Masama Mulla, lililoko Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, mwanamke mmoja mjasiriamali, Emili Ndossi (Mama Kadogoo), amejitosa kumaliza aibu hiyo, kwa kuingia mkataba na serikali ya kijiji wa miaka 15 ili kutoa huduma hiyo.
Kutokana na juhudi hizo za mama kadogoo, mfanyabiashara mashuhuri na mdau wa maendeleo wa Wilaya ya Hai, Shaban Mwanga, amemuunga mkono kwa kuchangia Sh.250,000 kumalizia uwekaji wa dari (sailing board) na mahitaji mengine ya choo hicho.
Akizungumza jana katika Soko la Masama Mulla, alipokwenda kuzindua choo hicho, mfanyabiashara na mdau huyo wa maendeleo, amesema choo hicho kilikuwa ni kilio cha akina mama wa Masama na wafanyabiashara wa soko hilo kwa muda mrefu.
“Aliyejenga choo hiki (Mama Kadogoo) wakati wa kukizindua alionyesha deficit (pengo la fedha), kwamba anahitaji la takribani shilingi 255,000. Ukiangalia kuna vitu vingi vinahitajika hapo, na mimi nadhani nitamkabidhi hapa fedha hizi, ili aweze kumalizia hicho choo kwa maana ya kuweka sailing board, kwa ajili ya kuongeza ustaarabu wakati akina mama na akina baba wanapokuja kujisaidia hapa waweze kujisitiri kwa kupata huduma sehemu safi sana.
…Kubwa zaidi, ni kuhakikisha tunamsaidia Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mama shujaa pekee nchini Tanzania, Afrika na Duniani kote. Kwa hiyo akina mama hawa, ukiwaunga mkono wanafanya mambo makubwa sana kama ambayo amefanya huyu mama wa Soko la Mulla.”
Awali, Mama Kadogoo, alimweleza Mfanyabiashara huyo (Shaban Mwanga) kuwa: “Hili soko kwa muda mrefu lilikuwa halina choo na watu walikuwa wanajisaidia migombani, tukaamua kuja na choo cha kisasa.
Zaidi alifafanua, “Choo ni cha matundu manne, wanaume matundu mawili, wanawake yako mawili. Kina bafu la wanawake kuogea tena kwa maji ya juu na bafu ya wanaume kuoga wa maji ya juu.
Nina vitu sijamaliza ambavyo nahitaji kuvipata, ni kuweka ‘sim tank’ juu ili maji yakikatika choo kiwe na maji ya uhakika na ya kutosha. Nimepiga hesabu kuanzia saruji mpaka vyuma, gharama yake inaenda karibu milioni mbili.”
Akieleza furaha yake baada ya kuzinduliwa choo hicho, mmoja wafanyabiashara wadogo sokoni hapo, Rahel Frank, Mkazi wa Masama Mbweera, amesema kwa miaka 40 wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la huduma ya choo.
“Kero tuliyoko nayo sana sana kwa hapa sokoni, kipindi cha mvua soko ni chafu, hasa tunapopeleka ndizi sokoni, bodadoda ambazo tunapishana nazo na magari makubwa (malori) ambayo yana shuka sokoni, wale tuliobeba ndizi kwa kichwa tunateseka sana.
“Kipindi ambacho kulikuwa hakuna choo tulikuwa tunateseka, hata kipindi cha mvua hatuna pakwenda kujisaidia, hasa unapokuwa tumbo limechafuka.
…Tunamshukuru Mama Kadogo, kwa juhudi zake amejitahidi kutukomboa sisi ambao wafanyabiashara wa Soko la Mulla, kwa kutujengea choo. Tunashukuru kwa huu mradi wa choo.”amesema Rahel.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED