Tanzania, ikiwa ni Kiongozi wa Utalii wa Safari Duniani na makazi ya Serengeti, Hifadhi Bora ya Taifa Duniani, inaungana na mataifa mengine kusherehekea Siku ya Wanyamapori Duniani leo Machi 03,2025.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza jukumu letu la kuhifadhi urithi wa wanyamapori kwa vizazi vijavyo: “Tumerithishwa, Tuwarithishe.” Tanzania imebarikiwa kuwa na bioanuwai tajiri inayojumuisha mamia ya aina za wanyamapori na mazingira ya kipekee, yanayovutia wageni kutoka pande zote za dunia.
Katika kuadhimisha siku hii muhimu, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inasisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi wanyamapori na maliasili kwa maendeleo endelevu ya sekta ya utalii na ustawi wa taifa kwa ujumla.
“Wanyamapori ni kipaumbele chetu, na kuwalinda ni jukumu letu. Tanzania itaendelea kusimamia uhifadhi endelevu ili kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinaweza kufurahia urithi huu wa thamani,” imesema Bodi ya Utalii Tanzania.
Kwa miaka mingi, Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika uhifadhi wa wanyamapori kupitia hifadhi zake za taifa, mapori ya akiba na maeneo ya urithi wa dunia kama Serengeti na Ngorongoro. Serikali, sekta binafsi na jamii zinaendelea kushirikiana kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinaendelea kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Katika Siku hii ya Wanyamapori Duniani, tunatoa wito kwa Watanzania na dunia kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuhifadhi wanyamapori. Kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa Unforgettable.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED