Tanzania yapokea Faru Weupe 18 kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya uhifadhi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:25 PM Mar 04 2025
Faru Weupe wawili kati ya 18 kutoka Afrika Kusini wakiwa katika hifadhi ya Ngorongoro.
Picha: Mpigapicha Wetu
Faru Weupe wawili kati ya 18 kutoka Afrika Kusini wakiwa katika hifadhi ya Ngorongoro.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa mara ya kwanza imepokea Faru Weupe 18 kutoka Afrika Kusini kwa lengo la kuimarisha uhifadhi nchini.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo Machi 4, 2025, katika Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, amesema kuwa mradi wa kupandikiza faru hao ni hatua muhimu katika juhudi za uhifadhi nchini.

"Mradi huu wa kupandikiza Faru Weupe ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ni jitihada za serikali katika kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na unatekelezwa kwa mara ya kwanza kupitia makubaliano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kampuni ya AndBeyond," amesema Chana.

Ameeleza kuwa katika makubaliano hayo, kampuni ya AndBeyond imechukua jukumu la kuwezesha upatikanaji na usafirishaji wa faru hao 18 kutoka Afrika Kusini kwa awamu ya kwanza. Awamu ya pili inatarajiwa kuleta faru wengine 18 ili kufikisha jumla ya faru 36, ambapo wengine watawekwa katika maeneo mengine ya uhifadhi nchini.

Chana amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za dhati za kukuza na kuimarisha sekta ya uhifadhi, ikiwa ni pamoja na mradi huu wa kupandikiza faru weupe.

Aidha, amebainisha kuwa Faru Weupe ni miongoni mwa wanyamapori walioko hatarini kutoweka na hivyo wameorodheshwa katika makundi yanayolindwa chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo Hatarini Kutoweka (CITES).

"Tanzania inaendelea kuunga mkono juhudi za kimataifa, hususan za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kwa kulinda wanyamapori hawa katika mazingira ya asili badala ya kuwafuga kwenye mashamba maalum au bustani," ameongeza Chana.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mbali na kuimarisha uhifadhi, Faru Weupe pia watatumika katika elimu ya jamii kuhusu usimamizi wa wanyamapori, kuendeleza tafiti za kisayansi na kuboresha mbinu za uhifadhi wa spishi hiyo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk. Elirehema Doriye, amesema kuwa kupokelewa kwa faru hao ni uthibitisho wa dhamira ya Tanzania katika kulinda spishi zilizoko hatarini kutoweka.

"Faru hawa watachangia juhudi za kimataifa za uhifadhi, kuongeza fursa za tafiti na kitaalamu, kukuza utalii, na kuinua uchumi wa jamii. NCAA imejipanga kuhakikisha usalama wao," amesema Dk. Doriye.

Naye, Mwakilishi wa Viongozi wa Kimila kutoka Afrika Kusini, iNkosi Zwelinzima Gumedeunywano, amesema kuwa lengo la kutoa faru hao kwa Tanzania ni kusaidia juhudi za uhifadhi na kuongeza uzalishaji wa faru katika Afrika Mashariki.

"Tafiti zinaonyesha kuwa Faru Weupe watastawi na kuzaliana vizuri katika eneo la Ngorongoro," amesema Gumedeunywano, akisisitiza kuwa Afrika Kusini iko tayari kushirikiana na Tanzania katika juhudi za uhifadhi wa spishi hiyo.