TUME ya Madini, imesema imeendelea kuimarisha ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo ya kati na mikubwa.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, alisema hayo jijini Dodoma, wakati akieleza mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Vile vile, alisema wanafanya ukaguzi katika ujenzi na matumizi salama ya mabwawa ya topesumu (TSF) pamoja na uhifadhi wa miambataka (WRD).
“Katika kipindi kinachorejewa, Tume ya Madini ilifanikiwa kufanya kaguzi katika migodi mikubwa saba ya uchimbaji wa madini iliyopangwa kukaguliwa katika mikoa sita ya kimadini.
Mikoa hiyo ni Mara, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Geita na Mtwara sambamba na kufanya kaguzi 187 katika migodi ya kati nchini,” alisema.
Pia, alisema katika kipindi rejewa, Tume imefanikiwa kufanya ukaguzi katika masuala ya usalama, afya, mazingira katika migodi midogo 60,761 iliyopo katika mikoa 26 ya kimadini.
Alisema mikoa hiyo ni Morogoro, Tabora, Arusha, Kahama, Mwanza, Tanga, Manyara, Iringa, Njombe, Mbogwe, Shinyanga, Dodoma. Kigoma, Kagera, Chunya, Geita, Mara, Mbeya, Rukwa, Lindi, Ruvuma, Mtwara, Songwe, Pwani, Dar es Salaam na Katavi.
Alisema mapungufu yaliyobainika katika kaguzi hizo, wahusika walielekezwa kuyafanyia kazi mapungufu hayo kwa kuzingitia matakwa ya Sheria ya Madini Sura ya 123.
“Katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Februari, 2025, ukaguzi ulifanyika katika maghala ya kuhifadhia baruti kwenye mikoa 30 ya kimadini, bohari 164, Stoo 268 na masanduku 207 yalikaguliwa,” alisema.
Alisema, mafunzo kuhusu masuala ya usalama, afya, mazingira pamoja na usimamizi wa baruti yalitolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini katika mikoa mbalimbali ya kimadini nchini na wachimbaji 11,478 walishiriki.
“Katika kuelimisha umma na kuboresha mawasiliano kati ya Tume ya Madini na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini, Tume imefanikiwa kufanya utayarishaji wa vipindi maalum na makala zinazohusu maudhui ya ndani.
“Na mchango wa kampuni za uchimbaji madini katika jamii kupitia programu za CSR katika Mikoa mbalimbali ya kimadini nchini kwa njia ya redio na luninga pamoja na kuchapishwa katika tovuti na mitandao ya kijamii,” alisema.
Hata hivyo, alisema vipindi hivi vimeendelea kuelimisha umma kuhusu masuala ya madini nchini, ili kufungua fursa kwa Watanzania kunufaika na rasilimali madini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED