“Usipopata muamala ndani ya saa mbili ruksa kushtaki benki”

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 03:47 PM Feb 27 2025
Ofisa Mwandamizi Mkuu, Mifumo ya Malipo ya Taifa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kidee Mshihiri.
Picha: Salome Kitomari
Ofisa Mwandamizi Mkuu, Mifumo ya Malipo ya Taifa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kidee Mshihiri.

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kuwa malipo ya benki moja kwenda nyingine yanapaswa kukamilika ndani ya saa mbili, na ikiwa mteja hajapata fedha yake ana haki ya kuishtaki benki husika kwa kuwa analindwa na sheria.

Akiwasilisha mada ya mifumo ya fedha, Ofisa Mwandamizi Mkuu, Mifumo ya Malipo ya Taifa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kidee Mshihiri, amesema mfumo wa kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine unaitwa Interbank Settlement System (TISS) ambao umeimarishwa.

Amesema kumekuwa na tabia ya mteja kuambiwa tatizo liko BoT ndio maana hapati malipo yake, jambo ambalo si kweli kwa kuwa BoT inaona tu haiwezi kufanya chochote kwenye muamala wa mtu kwa kuwa benki zote za biashara akaunti zao zipo Benki Kuu.

“Unakuta mtu ameenda benki X amehamisha fedha kwenda benki nyingine akifika kule anaambiwa hakuna fedha, akirudi kwenye benki alitohudumiwa anaambiwa tatizo liko BoT, jambo ambalo si sahihi.Ukiamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine lazima ndani ya saa mbili upate,”amesema.

Aidha, amesema BoT kuna dawati maalum la wateja na mtu yeyote anaruhusiwa kuwasilisha malalamiko yake na BoT itashtaki kwa niaba ya mteja, hivyo wananchi watambue ipo sheria inawalinda na wanaruhusiwa kuzishtaki benki.

Kidee amesema wateja wengi wameshasaidia na dawati la malalamiko ya wateja lililopo BoT, huku akitolea mfano wa mteja mmoja mkulima wa pamba ambaye Sh. Milioni 15 zilitolewa kwenye akaunti yake bila idhini yake, lakini alivyoenda benki alisumbuliwa kwa muda mrefu,alikuja kwetu na tulimsaidia na akalipwa ndani ya saa 2.

Aidha, amesema benki hazitakiwi kutoa siri za wateja na kwamba namna zinavyofanyakazi nis awa na siri ya mgonjwa na daktari ambayo haitakiwi kutoka.

“Hairuhusiwi mteja kwenda benki na kujua taarifa za akaunti ya mteja mwingine, huwezi kuuliza huyu kanilipa kiasi hiki lakini sijapata hebu angalia kama kwenye akaunti yake kuna fedha au la, hayo hayaruhusiwi,”amebainisha.