Vyama vya Ushirika nguzo ya kumuinua mwanamke kiuchumi

By Getrude Mpezya , Nipashe
Published at 03:54 PM Mar 05 2025
Vyama vya Ushirika kuwa nguzo ya kumuinua mwanamke kiuchumi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Vyama vya Ushirika kuwa nguzo ya kumuinua mwanamke kiuchumi.

Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Kaimu Naibu Mrajis wa Ushirika - Uhamasishaji, Consolata Kiluma, amewataka wanawake kutumia vyama vya ushirika kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi.

Amesema kuwa vyama vya ushirika, hususan vya Akiba na Mikopo (SACCOS), ni sehemu salama kwa wanawake kuhifadhi fedha zao na kupata mikopo yenye riba nafuu, hali inayowasaidia kupata mitaji kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya kiuchumi.

Kiluma alitoa wito huo alipotembelea mabanda ya vyama vya ushirika vya ELCT-SACCOS na Arusha Women in Business katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Arusha.

Neema Mcharo, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la vyama vya ushirika, amesema amejifunza umuhimu wa kuweka akiba na amana kupitia vyama vya akiba na mikopo. Amehimiza wanawake wengine kujifunza kupitia vyama hivyo ili kujenga msingi wa maendeleo yao ya kifedha.

"Nimefurahishwa na maonesho haya kwani nimepata elimu kuhusu kuweka akiba na kukopa kupitia vyama vya ushirika. Nawahamasisha wananchi wenzangu kufika kwenye banda la ushirika ili nao wajifunze," amesema Neema.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2025 kitafanyika jijini Arusha chini ya kaulimbiu: "Wanawake na Wasichana 2025: Imarisha Usawa, Haki na Uwezeshaji."