Wafanyakazi Wenye Mahitaji Maalumu wanufaika na ujumuishaji kazini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:11 PM Apr 29 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu  Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ametembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi 2025 yanayoendelea mkoani Singida ambapo amekutana na kuongea na wafanyakazi wenye mahitaji maalumu ambao ni waajiriwa wa WCF.

Watumishi hao walimueleza Kikwete namna WCF inavyowajumuisha kikamilifu katika kila hatua na matukio yote yanayohusisha wafanyakazi na kuwawezesha kwa kuwapatia vifaa wezeshi vinavyowarahisishia kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Nilipoanza kazi WCF, waliniuliza vifaa ninavyohitaji katika kutekeleza majukumu yangu, ambapo niliwaeleza na nilipatiwa vifaa hivyo na kwa sasa ninaendelea kutekeleza mjukumu yangu kikamilifu” Alieleza Bw. Emmanuel Mhehwa ambaye ni Afisa Matekelezo Ofisi ya WCF-Kinondoni

Waziri Kikwete aliipongeza WCF kwa jitihada za kuimarisha usawa na ujumuishaji mahali pa kazi, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na huduma bora zaidi kwa wafanyakazi wote.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF Dk. Abdulsalaam Omar, alimuhakikishia Waziri kuwa WCF itaendelea kuwajumuisha wafanyakazi wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha kwamba mazingira yao ya kazi yanakuwa salama kama ilivyo kwa wafanyakazi wote.