Watalii 37,614 raia wa Uholanzi wameitembelea Tanzania

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:03 PM Mar 13 2025
Watalii 37,614 raia wa Uholanzi wameitembelea Tanzania.

ZAIDI ya watalii 37,614 kutoka nchini Netherlands, wameitembelea Tanzania mwaka 2024, huku serikali ikieleza siri ya kupokea watalii hao kwa wingi kutoka taifa moja, kunatokana na kuwapo kwa safari za ndege kwa siku sita za wiki, ambazo ni za moja kwa moja kutoka Netherlands mpaka Tanzania.

Akizungumza leo, Machi 13, 2025 katika Jiji la Amsterdam (Uholanzi) na ujumbe wa Kampuni zaidi ya 30 za Tanzania zinazotoa huduma mbalimbali katika sekta ya utalii pamoja na wauzaji na wanunuzi wa bidhaa za huduma za utalii nchini Netherlands, Balozi wa Tanzania katika Falme ya Netherlands, Caroline Chipeta, amesema makundi hayo yanakutana kufanya mazungumzo ya kibiashara.

Balozi Chipeta, amesema pamoja na mambo mengine, mkutano huo unatangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini.

“Leo niko hapa Amsterdam (Uholanzi), katika msafara unaotangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchibni Tanzania. Msafara huu, unawakutanisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa za huduma za utalii.

“Lakini pamoja na hayo unatangaza pia, vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini Tanzania. Msafara huu wa kutangaza utalii unajumuisha Kampuni zaidi ya 30 kutoka Tanzania zinazotoa huduma mbalimbali katika sekta ya utalii.”

Aidha, Balozi Chipeta, amesema matokeo hayo ni juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania, kupitia ofisi ya Ubalozi hapa Netherlands, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali walioko nyumbani Tanzania, lakini pia na wadau walioko Netherlands, ambao wanaendelea kuitangaza Tanzania.