Waziri Jafo aagiza operesheni maalum kudhibiti bidhaa feki,biashara haramu Kariakoo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:56 PM Mar 17 2025
Waziri Jafo aagiza operesheni maalum kudhibiti bidhaa feki,biashara haramu Kariakoo

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jafo, ameagiza kuanza kwa operesheni maalum ya kufuatilia malalamiko kuhusu uwepo wa bidhaa feki na wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara haramu.

Agizo hilo limetolewa leo, Machi 17, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati Waziri Jafo akipokea ripoti ya uchunguzi kutoka kwa wajumbe wa kamati maalum iliyochunguza biashara za wafanyabiashara wa kigeni, hasa katika eneo la Kariakoo.
TBS na FCC Kuanza Operesheni ya Pamoja

Waziri Jafo ameielekeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani (FCC) kushirikiana katika operesheni hiyo maalum ili kuhakikisha bidhaa zinazouzwa nchini zinazingatia viwango vya ubora na haziharibu biashara za wazawa.

“TBS na FCC wahakikishe wanashirikiana kufuatilia malalamiko ya bidhaa zisizo na ubora zinazoharibu soko na uchumi wa ndani. Lengo letu ni kulinda maslahi ya Watanzania na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa nchini zinakidhi viwango vya ubora,” amesema Waziri Jafo.

Tahadhari Dhidi ya Biashara Haramu

Waziri Jafo pia ameonya kuwa biashara zinazokiuka taratibu zimekuwa changamoto kubwa nchini, huku baadhi ya vijana wa Kitanzania wakitumiwa katika mazingira yanayoweza hata kuhatarisha usalama wao.

"Kufanya kazi kinyume na taratibu ni changamoto kubwa. Vijana wanatumiwa kwa maslahi ya wengine, hali inayoweza hata kuwahatarishia maisha yao,” ameongeza.

Majina ya Vigogo Waliotishia Kamati Kuwasilishwa Kwa Mamlaka

Aidha, Waziri Jafo amepokea taarifa iliyobeba majina ya watu waliokuwa wakitishia kamati hiyo ili kuzuia uchunguzi wake. Ameahidi kwamba taarifa hiyo itabaki kuwa siri na itawasilishwa kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi.

"Nishukuru sana kwa taarifa hii. Mmeileta kwa majina ya wahusika waliotishia kamati. Kwa kuwa hii ni taarifa ya siri, nitaiwasilisha kwa mamlaka zinazohusika ili ijulikane namna gani kazi hii inakwamishwa,” amesisitiza.