Rais Ruto: Wanaotaka kupindua serikali wajaribu!

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:19 PM Jul 09 2025
news
Picha Mtandao
Rais wa Kenya William Ruto.

RAIS wa Kenya William Ruto ametoa onyo kali kwa wale anaoamini kwamba wanapanga kuiangusha serikali yake, akiachana na wito wake wa awali wa utulivu na mazungumzo, na kwamba kwa ujasiri aliwakaribisha wale wanaotaka kupindua serikali kujaribu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Rais Ruto ametoa matamshi hayo yaliyojaa ujasiri na mamlaka isiyopingika leo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Makazi ya Polisi katika Kituo cha Kilimani, Nairobi.

Katika hotuba ambayo haikuacha mashaka yoyote kuhusu msimamo wake, Ruto aliwahutubia moja kwa moja wanasiasa fulani na kundi la vijana Wakenya wengi wao kutoka vuguvugu la Gen Z walioko mstari wa mbele katika maandamano ambao alisema wanatishia kumuondoa madarakani kwa njia isiyo ya kikatiba.

“Nataka kusema na hawa viongozi waliokata tamaa. Niliwaona wakisema hawatasubiri hadi 2027 wapige kura. Eti wanataka kuchochea vurugu, kuandaa maandamano, kuchoma mali ya watu, na kusababisha ghasia ili wapindue serikali kabla ya 2027. 

“Nataka kuwaambia, wajaribu! Watajua hawajui lolote! Jaribuni! Hii ni Kenya, taifa la kidemokrasia jamani,” Rais Ruto amesema kwa sauti ya ukakamavu na changamoto.

Kauli zake zinakuja wakati taifa hilo likikumbwa na wimbi la maandamano yanayoongozwa na vijana kote nchini humo, yaliyochochewa na hasira kuhusu uongozi na ukatili wa polisi.