SERIKALI ya Zambia imewasilisha mahakamani maombi ya kusitisha mazishi ya faragha ya Rais mstaafu Edgar Lungu, yaliyotakiwa kufanyika Afrika Kusini, leo, Juni 25, 2025.
Kesi hiyo imesikilizwa kwa saa moja, kabla ya ibada ya mazishi yake kuanza.
Serikali ya Zambia inataka Lungu afanyiwe mazishi ya kitaifa nyumbani, kitu kinachopingwa na familia ya Lungu, kutokana na kile kilichoelezwa ni uadui wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu kati yake na Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema.
Wanafamilia ya Lungu waliokuwa wamevalia nguo nyeusi kwa ajili ya mazishi, walikwenda hadi mahakamani jijini Pretoria, Afrika Kusini, kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi hiyo ambayo ingeamua kama anaweza kuzikwa.
Bado haiko wazi ni lini jaji atatoa uamuzi.
Lungu, ambaye aliongoza Zambia kati ya 2015 hadi 2021, alifariki dunia hospitalini nchini Afrika Kusini Juni 5, 2025 akiwa na miaka 68, kwa ugonjwa ambao haujawekwa bayana.
Maziko ya kitaifa nchini Zambia yalifutwa mara mbili, kwa sababu ya kutokubaliana juu ya mipango ya mazishi, kati ya familia na serikali.
Familia yake na wanasheria wanasema aliacha maagizo maalum kwamba hatataka Hichilema kuhudhuria mazishi yake, wakati serikali ya Zambia ikisema Hichilema alitakiwa kuongoza mazishi ya kiserikali.
Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha, aliwasilisha maombi hayo kwenye mahakama jijini Pretoria, Afrika Kusini jana Juni 24, 2025 iliyotaka zuio la haraka la mahakama la mazishi yaliyotarajiwa kufanyika leo, Juni 25, 2025.
Shirika la Utangazaji la Taifa la Zambia (ZNBC), limeripoti kuwa maombi hayo yanataka rais huyo wa zamani azikwe nchini Zambia kwa heshima kamili za kijeshi, kama ilivyoagizwa kwenye sheria za Zambia na kwa kuzingatia kwa maslahi ya umma.
Familia inasema kuwa ibada ya mazishi ya Lungu, ilitarajiwa kufanyika katika kanisa moja jijini Johannesburg, takribani kilomita 60 kutoka Pretoria na maziko yake yangefanyika kwa faragha.
Chanzo: DW
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED