MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, amezindua rasmi jengo jipya la ofisi ya taasisi hiyo wilayani Kishapu.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Juni 25, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wananchi na Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo.
Chalamila akizungumza wakati wa uzinduzi huo, amesema ofisi hiyo mpya itachochea utendaji kazi kwa ufanisi, pamoja na wananchi kufika kwa wingi kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya rushwa.
"Shukrani kwa Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza TAKUKURU kwa rasilimali watu, vitendea kazi na ujenzi wa ofisi, ili kuboresha huduma bora kwa wananchi," amesema Chalamila.
Amesisitiza kutunzwa kwa jengo hilo, pamoja na watumishi kufanya kazi kwa weledi, ili kutokomeza rushwa.
Aidha, ametoa wito kwa shule zote za msingi na sekondari, kuanzisha Klabu za Wapinga Rushwa, ili kujenga taifa la watu wazalendo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, amesema wananchi watafika kwa wingi kutoa taarifa za rushwa, sababu ofisi ipo katika mazingira rafiki, tofauti na ilivyokuwa kwenye jengo la kupanga na wakikosa uhuru.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Boniphace Butondo, amesema TAKUKURU ni chombo muhimu kwa maendeleo ya taifa na kumpongeza Rais Samia, kwa ujenzi huo.
Mkurugenzi wa Milki Mhandisi Dk. Emmanuel Kiyabo, akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, amesema lilianzishwa Januari 27, 2024 na kwamba hadi kukamilika limetumia Sh. milioni 438.3.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED