Wadau wa elimu wahimizwa kusaidia wenye uhitaji

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 05:10 PM Sep 22 2025
news
Picha Shufaa Lyimo
Uongozi wa Shule ya Mzambarauni wakishirikiana na wadau kukata utepe ishara ya kuzindua madarasa yaliyokarabatiwa.

WADAU wa elimu wameombwa kusaidia kwa kuchangia wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia Kompyuta ya kujifunzia, Tehama pamoja na kuwajengea chumba maalum cha upimaji wa masikio.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa kitengo cha viziwi wa shule ya Msingi Mzambarauni iliyopo  Gongo la Mboto mkoani Dar es Salaam, George Njau wakati alipokuwa kwenye hafla ya uzinduzi wa madarasa yaliyokarabatiwa pamoja na kupokea vifaa vya shule.

Njau amesema upatikanaji wa vifaa hivyo utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto waliokuwa nayo wanafunzi hao. 

“Tunashukuru klabu hizi kwa kusaidia kukarabati madarasa saba pamoja na vifaa vya shule, kwa kuwa itawasaidia wanafunzi kusoma kwenye mazingira mazuri vile vile ufaulu utazidi kuongezeka,” amesema.

Amesema shule hiyo ina wanafunzi 180, ambapo kati yao 80 ni wa kutwa na 80 wanarudi nyumbani, akisema ukarabati huo utapunguza utoro kwa kiasi kikubwa shuleni hapo. 

Naye Rais wa Klabu ya Rotary, Reshma Shah amesema wamelazimika kukarabati madarasa saba pamoja na kutoa msaada wa vifaa vya shule kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum wapate elimu bora. 

“Tumechukua hatua hiyo kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wenye uhitaji maalum wanapata elimu kwenye mazingira safi na salama ili waweze kupata matokeo mazuri,” amesema. 

Amesema mazingira ya shule yakiwa mazuri yatawasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.

Mwanafunzi wa Shule hiyo Maliki Abdul, amesema anawashukuru wadau wote kwa msaada waliowapatia kwakuwa utawasaidia kusoma kwa bidii. 

“Msaada na ukarabati huu utatufanya sisi wanafunzi tusome kwa bidii vile vile kwa wale ambao walikuwa hawapendi shule watabadilika,” amesema Abdul.