Serikali yaahidi kuimarisha SACCOS kuchochea maendeleo ya wananchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:54 AM Oct 03 2025
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, amesema Serikali itaendelea kuimarisha na kusimamia Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) nchini ili viwe chachu ya kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Mwandumbya alitoa kauli hiyo hivi karibuni jijini Arusha, wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa mwaka 2024.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dk. Benson Ndiege, alisema sekta ya SACCOS inaendelea kukua na kuimarika nchini, hali inayothibitishwa na ongezeko la mali na mikopo inayotolewa.

Kwa mujibu wa Dk. Ndiege, mali za SACCOS zimeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.32 mwaka 2023 hadi shilingi trilioni 1.46 mwaka 2024, huku utoaji wa mikopo ukipanda kutoka shilingi trilioni 1.1 mwaka 2023 hadi kufikia trilioni 1.20 mwaka 2024.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Kilimo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (SCCULT), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), TFC, COASCO, DSIK pamoja na SACCOS husika.