Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ameeleza namna alivyopata mafunzo ya uzalendo kupitia Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Rashidi Mfaume Kawawa, kwa ushauri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Akihutubia wananchi leo (Oktoba 3) katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Liwale, mkoani Lindi, Dk. Nchimbi amesema mara baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kwa mara ya kwanza, Mwalimu Nyerere alimwita na kumwelekeza kutafuta mafunzo ya uzalendo kutoka kwa Kawawa.
“Nilipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Mwalimu Nyerere aliniita akanambia, kama unataka kuwa mzalendo, kaa na Mfaume Kawawa akufundishe. Wakati huo Kawawa alikuwa Kamanda wa UVCCM,” amesema Nchimbi.
Akiendelea na simulizi yake, amesema kumbukumbu kubwa aliyobeba kutoka kwa Kawawa ni wakati alipomtembelea hospitalini Desemba 2009, kipindi ambacho kiongozi huyo alikuwa mgonjwa.
“Nilienda hospitalini kumsalimia, baada ya siku chache akanipigia simu akaniita tena. Nilipofika tulikuwa wanne; mimi, mtoto wake Victor Kawawa, Zainab Kawawa na mlinzi. Akanambia wazi kwamba hatapona. Pia akanisisitizia kuhakikisha chama kinabaki kuwa cha watu, kinawatetea wenye shida, na kiwe kimbilio la wanyonge. Haikupita wiki, mzee Kawawa alifariki dunia,” amesema Dk. Nchimbi.
Ameongeza kuwa kauli na urithi huo wa kisiasa ataendelea kuuenzi, na kwamba CCM itaendelea kusimama kama chama cha kuwatetea wanyonge na kuhakikisha wananchi wote wanapata hifadhi ya kijamii na kisiasa kupitia sera zake.
“Maneno na matendo ya Mzee Kawawa ni urithi wa thamani. CCM itaendelea kumuenzi na kuyaishi kwa vitendo ili kiwe chama cha watu na kimbilio la wanyonge,” amesisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED