Mfanyabiashara na mdau wa maendeleo ya elimu, Shaban Mwanga, ameishauri shule kongwe ya kitaifa ya Ufundi Moshi, kuanzisha mchakato wa kumiliki kiwanda chake cha uzalishaji wa bidhaa za ngozi, kitakachokuwa kikijenga uwezo kwa wanafunzi wenye uziwi nchini.
Akizungumza leo Oktoba 3, 2025 katika mahafali ya 54 ya shule hiyo, amesema alichokiona, baada ya kukagua bunifu za wanafunzi wa shule hiyo, kupitia bidhaa za ngozi, ni namna walivyo na uwezo mkubwa wa kubadilisha mazingira halisi ya darasani kwenda kwenye uhalisia.
“Kikubwa ambacho tumeona ni vile wanavyobadilisha mazingira halisi ya darasani kwenda kwenye uhalisia. Mfano tumeona jinsi wanaweza kufanya recycling (urejelezaji) wa vitu mbalimbali kwenda kwenye productive materials (bidhaa halisi); na tumeona wanafunzi wenye uwezo wa kushona, uwezo wa kutengeneza vitu kama sandles, viatu na mikoba.
…Nikaona sasa, kuna haja ya kuishauri shule ikatafuta wadau ambao wanaweza wakasaidia kufungua kiwanda kidogo ndani ya Moshi Technical, wakishirikiana na viwanda vya nje; hususani hapa Moshi, kuna kiwanda cha ngozi, ambacho kinatengeneza leather products."
Kwa mujibu wa Mwanga, wakiweza kushirikiana na Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd, wazazi wanaweza wakanufaika na wanafunzi wakanufaika kwa ajira.
Kutokana na bunifu za bidhaa hizo, Mwanga, ameahidi kubeba bajeti ya kugharamia mahitaji ya walimu wanaoenda masomoni kwa ajili ya mafunzo ya amali kwa wenye uziwi.
Aidha, mdau huyo wa maendeleo ameahidi kuipatia shule hiyo kompyuta mpya 40 kwa ajili ya kusaidia Teknolojia ya Habari na Mawasilaino (TEHAMA).
“Kwa awamu ya kwanza, naahidi kuwapatia kompyuta 40 kati ya kompyuta 60 zilizoko shuleni hapa, japo 40 pia ni chache; na zikitakiwa kuongezwa pia nitawaongezea. Kwa wastani wa Meshi Technical, mnatakiwa muwe na wastani wa kompyuta zisizopungau 200.
Zaidi ameongeza, “Hapo ndipo mnapoweza kusema sasa hawa watoto wanasoma. Shida yangu ni kwamba, tukiwaletea kompyuta 200 mnapakuziweka? Hiyo ni shida nyingine; hizo nyingine tuandae madarasa kwa maana ya miundombinu tuangalie ni jinsi gani ya kuwawezesha. Awamu ya pili kompyuta 50, awamu ya tatu, kompyuta hizo zilizobakia tutakuwa tumemalizia.”
Mkuu wa Shule hiyo, Philipo Mwanga, akifafanua kuhusu wazo hilo la kuwa na kiwanda chao cha ngozi, amesema katika hatua za awali kuelekea ndoto hiyo, tayari wameingia Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd, kwenda kujifunza na kufanya kwa vitendo kitu kinachowezekana, ili wanafunzi wa amali kujiimarisha kiufundi.
“Kwa sasa mipango yetu ni kuwa sehemu ya kiwanda cha ngozi katika nchi hii ya Tanzania. Ukitizama hapa sasa hivi tayari tuna pochi, tayari tuna viatu, tayari tuna vifaa mbalimbali, mikanda ipo, tayari tumeshaanza kwa kiwango kidogo.
…Lakini tunapoelekea sasa tunaelekea kuwa kiwanda kamili, kwa sababu tuna access kubwa ya kiwanda hiki cha Kilimanjaro Leather Goods, ambacho tayari tuna Memorandum of Understanding, kwamba muda wowote tunaweza kwenda pale kujifunza, kuchukua kitu kinachowezekana ili sasa kujiimarisha hapa shuleni.
“Kwa hiyo kwa upande huo tuna mikakati ya kuwa sehemu ya uzalishaji wa bidhaa nyingi za ngozi katika nchi hii na hasa tuanza kutumia mafunzo kwa wale wenye uziwi, ambao kwa kweli tumeona tuwape hiyo kwa sababu hawawezi sehemu nyingine, wanapata shida kutokana na changamoto yao, ukiwapeleka kwenye umeme, kwenye mbao zile mashine zinaweza kuwadhuru lakini mashine za kushona ngozi haziwadhuru.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED