Mradi wa Sh. mil 724 kuondoa adha wanakijiji kutumia maji na fisi

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 01:15 PM Oct 03 2025
 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, akimtwisha ndoo kichwani mkazi wa eneo hilo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, akimtwisha ndoo kichwani mkazi wa eneo hilo.

Wakazi 3,852 wa Kijiji cha Makuro, Wilaya ya Singida, hatimaye wameondokana na adha ya kutembea kilomita tisa kufuata maji machafu kwenye makorongo yanayotumiwa pia na fisi, baada ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha mradi wa maji safi wenye thamani ya Sh. milioni 724.

Wakizungumza kabla ya uzinduzi wa mradi huo uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, wakazi hao walieleza kuwa hali ya awali ilikuwa ngumu kwani walilazimika kushindana na wanyamapori kupata maji.

“Tulikuwa tunafuata maji kwenye makorongo ambayo pia yalitumiwa na fisi. Kukamilika kwa mradi huu ni mkombozi mkubwa sana, hata ndoa zetu sasa zitaimarika,” alisema Mwanahamisi Salum, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida, Lucas Said, alisema kukamilika kwa mradi huo kumeongeza kiwango cha upatikanaji maji safi wilayani Singida hadi asilimia 80.3. Aidha, alibainisha kuwa mkakati wa RUWASA ni kuongeza upatikanaji maji vijijini mkoani hapo kufikia asilimia 78.5 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, kutoka asilimia 71.3 ya sasa.

“Kiwango hiki tunaamini kitaongezeka zaidi mara baada ya kukamilika kwa miradi yote ya maji inayotekelezwa katika wilaya zote za mkoa wa Singida,” alisema Said.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua mradi huo, Mkuu wa Mkoa, Dendego, aliwataka kuulinda na kuutunza ili huduma hiyo iendelee kupatikana kwa muda mrefu. Pia aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji mkoani humo kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati kulingana na mikataba.

Vilevile, Dendego aliiagiza RUWASA kumlipa Sh. 500,000 mwananchi aliyejitolea eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa kisima cha maji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, alisema hadi sasa wamepokea kero 200 za wananchi kuhusu maji na kuzitafutia ufumbuzi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa urahisi.