Doyo aahidi soko la uhakika kwa wakulima wa mbaazi akipewa urais

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 02:19 PM Oct 03 2025
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassani Doyo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassani Doyo.

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassani Doyo, ameahidi kuwatafutia wakulima wa mbaazi soko la uhakika endapo atapewa ridhaa ya kuiongoza nchi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza leo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Stendi ya zamani, wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Doyo amesema changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa mbaazi ni mfumo wa stakabadhi ghalani, ambao kwa sasa umekuwa ukiwanyima wakulima faida stahiki.

Amesema wakulima wanahitaji soko huru litakalowapatia tija ya moja kwa moja, tofauti na mfumo wa sasa unaodhibiti bei na kumkandamiza mkulima wa kawaida.

“Mtakaponichagua, dhamana yangu ni kuhakikisha kila mkulima anapata soko la uhakika kwa asilimia 100. Nitahakikisha kila mkulima anauza mbaazi katika soko analolichagua mwenyewe, na siyo kulazimishwa kuuza kwa bei ya Sh. 400 kwa kilo kama ilivyo sasa chini ya CCM,” amesema Doyo.

Mgombea huyo ameongeza kuwa kilimo cha mbaazi ni sekta yenye tija kubwa kitaifa, lakini hakijawahi kuwanufaisha wakulima wadogo ipasavyo kutokana na mifumo isiyo rafiki kwao.