Ngorongoro kivutio maonyesho ya Magical 2025

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 05:09 PM Oct 03 2025
Ngorongoro kivutio maonyesho ya Magical 2025
Picha:Mpigapicha Wetu
Ngorongoro kivutio maonyesho ya Magical 2025

Wageni kutoka mataifa mbalimbali wametembelea maonesho ya utalii ya Magical yanayoendelea jijini Nairobi, Kenya, na kuonyesha kuvutiwa na vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji vinavyopatikana katika hifadhi ya Ngorongoro.

Maelezo yaliyotolewa kuhusu hifadhi hiyo yamewavutia wengi kutokana na upekee wake, ikiwemo uwepo wa wanyama maarufu wa “Big Five” na historia ya chimbuko la binadamu wa kale. Uwepo wa wanyama mbalimbali na mandhari ya kipekee ya hifadhi ya Ngorongoro kumeifanya kuwa kivutio kinachoshirikisha wapenzi wa utalii wa kimataifa.

Afisa Masoko Mkuu wa hifadhi hiyo, Michael Makombe, alisema ushiriki wa Ngorongoro katika maonesho hayo umeongeza wigo wa utambulisho wake kimataifa na kutarajia ongezeko kubwa la wageni wa kimataifa.

“Tunatarajia wageni wengi baada ya kumalizika maonyesho haya. Vivutio vyetu vimewavutia wengi sana, na kwa kweli tunatarajia ongezeko la wageni katika siku zijazo,” amesema Makombe.