Mhashamu Askofu Sarah Mullally ameteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury Muadhama Mkuu Sarah Mullally anakuwa ni mwanamke wa kwanza kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury.
Hivyo anakuwa Askofu Mkuu wa 106 kutoka kwa Askofu Mkuu Augustine aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Papa Gregory wa Rumi kuwa Askofu wa kwanza wa Canterbury mwaka 595, ikiwa ni miaka 1300 iliyopita tangu kuanzishwa kwa Kanisa nchini Uingereza.
Vyombo mbalimbali ya habari nchini Uingereza vimeripoti Uteuzi huo, historia inasema katika kipindi cha miaka 500 iliyopita ya mapokeo ya Kanisa hilo kuhusu kiti cha Canterbury, huyu anakuwa ni Askofu Mkuu wa kwanza mwanamke.
Kabla ya uteuzi huo, Saraha alikuwa Askofu wa London, dayosisi muhimu sana katika Church of England. Muadhama Mkuu Mullally anachukua nafasi ya Muadhama Mkuu Askofu Mkuu Justin Welby, aliyejiuzulu hivi karibuni.
Kwa uteuzi huo, Sarah Mullally atakuwa pia ni Mkuu wa Jimbo Kuu la Canterbury, Mkuu wa Kanisa la Uingereza (Kanisa Anglikana) na pia Mkuu wa Kanisa Anglikana Duniani (Worldwide Anglican Communion).
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Askofu Mkuu Emmaus Mwamakula, Kiongozi wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, ameandika ujumbe wa pongezi kwa Askofu Mkuu Mullally, akieleza kuwa uteuzi huo ni ushahidi wa ukuaji wa nafasi ya wanawake katika uongozi wa kiroho na kuimarika kwa usawa wa kijinsia ndani ya makanisa ya kikristo duniani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED