Vikosi vya ulinzi na usalama Mwanza vyafanya matembezi ya mazoezi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 04:39 PM Oct 03 2025
Vikosi vya ulinzi na usalama Mwanza vyafanya matembezi ya mazoezi
Picha: Mpiggapicha Wetu
Vikosi vya ulinzi na usalama Mwanza vyafanya matembezi ya mazoezi

Vikosi vya ulinzi na usalama mkoani Mwanza leo Oktoba 3, 2025 vimefanya matembezi ya pamoja (Route March) kwa umbali wa kilomita sita katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Mwanza, ikiwa ni sehemu ya mazoezi ya kawaida kwa ajili ya kuimarisha afya na mshikamano wa askari.

Matembezi hayo yameshirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji, Polisi Wasaidizi pamoja na Mgambo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa, amesema lengo la mazoezi hayo ni kuimarisha afya za askari, kukuza nidhamu, mshikamano na kuongeza utimamu wa miili ili wawe tayari kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Mazoezi haya ni muhimu sana kwa afya ya mwili na akili, lakini pia ni maandalizi ya kuhakikisha askari wapo tayari kulinda amani na usalama wa raia na mali zao,” amesema Mutafungwa, akisisitiza kuwa askari wote wanapaswa kushiriki kikamilifu mazoezi hayo endelevu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Vikosi vya Jeshi mkoani Mwanza, Kanali Said Mkenge, amewapongeza askari kwa moyo wa kujitolea na kukamilisha matembezi hayo, akibainisha kuwa mshikamano na ushirikiano baina ya vikosi ndiyo msingi wa ulinzi na usalama wa mkoa huo.

Naye Mkuu wa Kikosi cha MTC, Kanali Alley Mohamed, amesema mbali na kuboresha afya, mazoezi hayo yanajenga mshikamano, umoja na mawasiliano bora kati ya vikosi, jambo linaloongeza ufanisi wa utendaji kazi wao.