ACT yazidi kushika kasi Zanzibar, Othman atajwa kinara kizazi kipya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:54 AM Sep 29 2025
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman

Zanzibar imeelezwa kuwa taifa lenye historia kubwa na nafasi ya kipekee barani Afrika na duniani, lakini heshima hiyo haitadumu iwapo wananchi wake hawatasimama imara kulinda utu, haki na maendeleo yao.

Kauli hiyo imetolewa na Hassan Jani Masoud katika mkutano mkubwa wa hadhara wa chama cha ACT Wazalendo uliofanyika Bumbwini, Kaskazini B Unguja, uliovuta maelfu ya wananchi waliokusanyika kumsikiliza mgombea urais wa chama hicho, Othman Masoud Othman.

Akihutubia wananchi, Jani alihoji sababu za wananchi kuendelea kutaabika na ufukara licha ya uwekezaji mkubwa unaoonekana kila kona ya Zanzibar. Alisema chanzo kikuu cha changamoto hiyo ni ukosefu wa uadilifu kwa viongozi waliopo madarakani na miradi mingi kubaki kuwa njia ya ufisadi badala ya kuwanufaisha wananchi.

Jani alimtaja Othman Masoud kuwa kiongozi safi, mwenye historia ya misimamo thabiti na uzalendo wa kweli kwa Zanzibar, akisisitiza kuwa ndiye suluhisho la uongozi mpya unaohitajika kuijenga Zanzibar mpya. “Othman ana macho ya kuona mbali, si kiongozi wa muda mfupi bali wa kizazi kizima, anayepigania mustakabali wa taifa kwa vizazi vijavyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, alisema kiongozi yeyote anayepata nafasi bila ridhaa ya wananchi hawezi kuwatumikia ipasavyo. Alifafanua kuwa katika ziara zake, kila kijiji alichotembelea wananchi wamelalamikia kukosa maji safi na salama kwa zaidi ya miaka 60, hali inayoonesha wazi kutowajibika kwa watawala.

“Kinachoendelea ni ufisadi na dhulma, huku wananchi wakiachwa wakiteseka kila mahali. Zanzibar ni nchi ya wastaarabu, ina hata sheria za kulinda wanyama, lakini binadamu wanateseka kwenye nchi yao bila huruma yoyote,” alisema kwa masikitiko.

Othman aliongeza kuwa ni fedheha kubwa haki za Wazanzibari kunyimwa kila uchaguzi na wananchi kufanywa watumwa. Alikumbusha tukio la mwaka 2020 ambapo watu 21 waliuawa na vyombo vya dola ili kulazimisha utawala wa mabavu.

“Nasema wazi, watawala wa aina hii hawafai. Wanapaswa kukataliwa na kila mmoja wetu kwenye sanduku la kura Oktoba 29,” alisisitiza.

Akiendelea kuwahamasisha wananchi, Othman alisema zama za mateso kwa Wazanzibari zimefika mwisho na kila mmoja ana jukumu la kumshawishi mwenzake kukataa CCM.

“Tunasema wazi, mlilofanya mumeshafanya. Kwa sasa hatukubali tena. Tunataka kuona ustaarabu kwenye uchaguzi,” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu na umati wa wananchi.