Vikundi vya wanawake na vijana Arusha kupewa mikopo ya mamilioni kujikwamua kiuchumi

By Allan Isack , Nipashe
Published at 12:10 PM Sep 29 2025
Vikundi vya wanawake na vijana Arusha kupewa mikopo ya mamilioni kujikwamua kiuchumi
Picha:Mpigapicha Wetu
Vikundi vya wanawake na vijana Arusha kupewa mikopo ya mamilioni kujikwamua kiuchumi

Vikundi vya wanawake na vijana katika kata 25 za Halmashauri ya Jiji la Arusha vitawezeshwa kifedha kwa ajili ya kuendeleza miradi waliyoibuni na kuianzisha kwenye maeneo yao, ili kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yalibainishwa jana jijini Arusha na Mwenyekiti wa Taasisi ya Nasimama na Mama Tanzania Kanda ya Kaskazini,Monika Ligonela wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango huo.

Amesema taasisi hiyo itasimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo kilimo, ufugaji na ujasiriamali kwa lengo la kutoa matokeo chanya kwa wahusika ambao ndio walengwa wakuu katika kukuza uchumi wao.

“Mipango yetu ni kuhakikisha tunawawezesha na kuyajenga kiuchumi na kisiasa makundi ya vijana na wanawake katika jamii kwa lengo la kukuza vipato vyao na kujitegemea. Pia tunatoa mafunzo mbalimbali kwa makundi hayo wenye mrengo wa kujifunza masuala ya uraia na siasa nchini Tanzania ili kuwaibua watu watakaoweza kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa,” alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake, Katibu wa taasisi hiyo, Dionis Moyo, alisema kwa kuanza wanatarajia kukusanya Sh milioni 150 ambazo zitagawiwa kwa vikundi 15 vya kata husika, ambapo kila kikundi kitapatiwa Sh milioni 10 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kilimo, ufugaji na biashara ndogondogo.

“Tutaanza utekelezaji mara baada ya uzinduzi wa taasisi. Tunakaribisha pia vikundi vingine vitakavyobuni miradi ili viwe sehemu ya mpango huu, ikiwamo miradi ya ujasiriamali, ufugaji wa ng’ombe, kuku na kilimo,” alisema Moyo.

Akizungumza kwa niaba ya wadau, Ofisa wa Uhifadhi Kitengo cha Biashara kutoka Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Iddy Kasule, aliwataka wanawake na vijana kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.

Alisema taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya uhifadhi na pato la taifa kupitia shughuli za utalii, ambapo sehemu ya mapato yanayopatikana hutolewa kwa jamii zinazopakana na hifadhi pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Vilevile, Kasule alihamasisha wananchi na viongozi kuendeleza utalii wa ndani ili kuongeza mapato na kuchochea maendeleo ya jamii.