Waliomteka na kumuua mwanafunzi wa Mzumbe wakamatwa

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 03:10 PM Sep 29 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewakamata watuhumiwa wa utekaji na mauaji ya kikatili ya Shyrose Mabula (21), mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, Shyrose alitekwa Septemba 14, 2025 na mwili wake ulipatikana Septemba 16 katika Mtaa wa Moroviani, Kata ya Isyesye jijini Mbeya, ukiwa umechomwa moto.

Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na Marwa John (25), Edward Kayuni na Websta Mwantebele (27), ambao wamekiri kupanga njama za utekaji kwa lengo la kudai fedha kutoka kwa baba wa marehemu, Dk. Mabula Michael.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kupata fedha hizo, walimnywesha sumu aina ya Round Up, kumnyonga kwa kamba na kisha kuchoma mwili wake.

Kamanda Kuzaga amesema msako unaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine akiwemo mganga wa jadi aliyepokea baadhi ya vitu vya marehemu. Aidha, ametoa onyo kali kwa vijana na wananchi kuachana na tamaa ya mali kupitia vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa uhalifu haulipi.