Moto mkubwa umeteketeza bweni la wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Asha Rose Migiro, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, na kusababisha shule hiyo kufungwa kwa siku saba.
Moto huo ulizuka usiku wa kuamkia Septemba 29, wakati wanafunzi wakiwa darasani, na kuharibu mali zote za wanafunzi 374 waliokuwa wakitumia bweni hilo. Walimu waligundua moto mapema na kuomba msaada, lakini juhudi za kuuzima zilishindikana kutokana na kuenea kwa kasi kubwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Nurdin Babu, amesema wanafunzi wamebaki na nguo walizovaa pekee, hivyo wamepewa mapumziko ili kupata msaada wa kisaikolojia. Wanafunzi wa kidato cha nne na tano pekee ndio waliobaki shuleni kuendelea na masomo kutokana na ukaribu wa mitihani.
Katika tukio hilo, wanafunzi 32 walipata matatizo ya kupumua kutokana na kuvuta moshi na walikimbizwa Kituo cha Afya Mwilenge. Wengi walitibiwa na kuruhusiwa huku wanne wakibaki kwa uangalizi zaidi.
Babu ametoa wito kwa wazazi na wadau kujitokeza kusaidia wanafunzi waliopoteza mali zao, zikiwemo sare, madaftari, vitabu na vifaa vingine muhimu. Aidha, alisema chanzo cha moto bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea.
Kwa upande wake, Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi, amebainisha hakuna madhara makubwa ya kibinadamu yaliyotokea zaidi ya wanafunzi waliopata changamoto za kupumua. Ameongeza kuwa elimu ya kinga dhidi ya majanga ya moto itaendelea kutolewa mashuleni.
Mkoa wa Kilimanjaro umekumbwa na matukio kadhaa ya moto mashuleni katika miaka ya karibuni, ikiwemo Shule ya Wasichana Ashira mwaka 2021, Kaloleni mwaka 2023 na Sangiti mapema mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED