Samia: Tanga inarejea kuwa kitovu cha viwanda na ajira mpya

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:15 PM Sep 29 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema mwelekeo wake ni kuirejesha Tanga ya viwanda kupitia uanzishwaji wa kongani za viwanda na kufufua viwanda vilivyobinafsishwa, ikiwamo Kiwanda cha Chai Korogwe.

Akizungumza leo, Septemba 29, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Tanga Mjini, Samia amesema Bandari ya Tanga imepata uamuzi wa kimkakati wa kuwa bohari ya mafuta na gesi, hatua ambayo itazalisha ajira mpya 2,100 na kuinua uchumi wa wananchi wa Tanga.

“Mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga umekamilika kwa asilimia 84 na tayari umetoa ajira nyingi. Mfano, katika eneo la Chengereani watu 1,300 wameajiriwa na kwa jumla Tanga imezalisha ajira 2,000 kupitia mradi huu,” amesema.

Samia ameongeza kuwa serikali itaanza utekelezaji wa reli itakayounganisha Bandari ya Tanga na miji ya Arusha hadi Musoma, umbali wa kilometa 1,108, ili kufungua maeneo mapya ya viwanda na madini pamoja na kuongeza ajira.

Aidha, amesema serikali itapanua barabara kuu ya Dar es Salaam–Chalinze–Segera hadi Arusha yenye urefu wa kilometa 646, kutokana na msongamano mkubwa uliopo kwa sasa.

“Nimefurahi kuona kiwanda cha foma kimefufuliwa na kiwanda cha saruji kimeongeza uwezo wa uzalishaji. Pia tuna kiwanda kipya cha kufunga magari ya wagonjwa (ambulance). Tunataka kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza maeneo ya viwanda Tanga. Wito wangu ni kwamba maeneo ambayo hayatumiki yarudishwe ili wawekezaji wapate mazingira tayari,” amesisitiza.