Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara na nishati katika Jiji la Mwanza na mkoa mzima wa Kanda ya Ziwa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Akihutubia wakazi wa Mwanza kwenye mkutano wa kampeni, Doyo alisema barabara kuu ya Mwanza–Shinyanga itajengwa kwa kiwango cha lami na kupanuliwa kuwa barabara mbili za kisasa, hatua inayolenga kupunguza ajali za barabarani na kurahisisha safari za wananchi.
“Kwa heshima ya Jiji la Mwanza, tunapaswa kulifanya kitovu cha utalii na biashara. Utalii na biashara vitachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi. Tunataka iwe rahisi kwa wafanyabiashara kufika Mwanza na kusafiri kwa urahisi ili kuharakisha mzunguko wa uchumi,” alisema Doyo.
Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kujenga barabara za juu (flyover) katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa magari, ikiwemo Rock City, ili kupunguza foleni. Alibainisha kuwa Jiji la Mwanza linakua kwa kasi kiuchumi, hivyo linahitaji miundombinu ya kisasa inayorahisisha shughuli za wananchi.
“Tunakwenda kujenga barabara za juu ili kuondoa foleni kama ilivyo katika majiji mengine. Hii itarahisisha wananchi kuendelea na majukumu yao ya kila siku na kuchangia pato la taifa kwa hiari. Ni busara kumtengenezea Mtanzania mtandao rahisi wa ulipaji kodi,” alisisitiza Doyo.
Vilevile, ameahidi kuwa serikali ya NLD itajenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme ndani ya Ziwa Victoria kitakachozalisha zaidi ya megawati 2,000, hatua itakayosaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa nishati ya umeme katika kanda hiyo.
Baada ya mkutano huo, msafara wa mgombea huyo ulielekea Sengerema, Geita na Kigoma kuendelea na kampeni zake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED