Kesi ya ghorofa kuporomoka Kariakoo yatinga Mahakama Kuu

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 10:43 AM Sep 29 2025
Ghorofa lililoporomoka Karikaoo.

Kesi ya Ardhi namba 6075 ya mwaka 2025, inayowahusisha Kanari Swai na wenzake 49 dhidi ya wadaiwa mbalimbali, leo imewasilishwa katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, kwa ajili ya kusikiliza mapingamizi.

Awali, mawakili wa upande wa wadaiwa waliwasilisha pingamizi wakidai kuwa shauri hilo haliwezi kuendelea hadi mapingamizi hayo yatakapokuwa yamesikilizwa na kuamuliwa. Katika kesi hiyo, walalamikaji wanadai fidia ya shilingi bilioni 40 wakieleza kuwa walipata hasara kubwa kufuatia jengo la ghorofa kuporomoka na kusababisha madhara mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Wakili wa walalamikaji, Peter Madeleka, aliomba Mahakama isikilize shauri hilo kwa njia ya mdomo badala ya maandishi, akibainisha kuwa ni muhimu kwa Jaji kutoa maamuzi sahihi baada ya kusikiliza hoja za pande zote kwa moja kwa moja.