Dk. Mwinyi kukabidhi hatimiliki za mashamba ya mikarafuu Pemba

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 02:55 PM Sep 29 2025
Dk. Mwinyi kukabidhi hatimiliki za mashamba ya mikarafuu Pemba
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Mwinyi kukabidhi hatimiliki za mashamba ya mikarafuu Pemba

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kukabidhi hatimiliki za mashamba ya mikarafuu kwa wananchi Kisiwani Pemba.

Hatua hiyo inalenga kuwapatia usalama wa umiliki wananchi waliopatiwa mashamba ya mikarafuu na serikali, pamoja na wale waliorithi mashamba hayo kutoka kwa wazee wao lakini hawakuwahi kupewa hatimiliki rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani humo, Katibu wa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, alisema mpango huo utasaidia kuondoa na kuepusha migogoro ya ardhi inayohusiana na mashamba ya mikarafuu.

Alifafanua kuwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, serikali ilitoa maeneo ya ardhi kwa wananchi kwa ajili ya kilimo, ikiwemo kilimo cha mikarafuu, lakini wananchi hawakuwa na nyaraka za umiliki wa maeneo hayo.