Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amewataka wananchi wa Kanda ya Ziwa kutafakari kwa kina sababu zinazowafanya kubaki nyuma kimaendeleo licha ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kushika dola kwa zaidi ya miaka 60.
Akizungumza leo katika mkutano wa kampeni wilayani Sengerema, Doyo amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi wa Oktoba 29, atahakikisha wakulima wanapata fursa ya kuuza mazao yao kwenye masoko yenye tija na faida, badala ya kulazimishwa kuuza kwenye masoko yanayowanyonya na kuwaendeleza katika umaskini.
“Wananchi, mkiniamini na kunipa kura Oktoba 29, nitasimamia na kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na zenye motisha kwenye mazao yenu yote. Haiwezekani mtumie gharama kubwa katika kilimo halafu mpangiwe bei. Hizi ni mbinu za kuendeleza umaskini wenu ili CCM waendelee kuwatawala nyinyi na vizazi vyenu,” amesema Doyo.
Mbali na kilimo, mgombea huyo amezungumzia changamoto za huduma za kijamii na miundombinu wilayani Sengerema, akibainisha kuwa taifa lina rasilimali nyingi ikiwemo dhahabu, almasi na tanzanite, lakini bado wananchi wake wanaendelea kuishi maisha ya umaskini.
“Nchi hii ina madini ya kila aina, lakini wananchi wake hawana maji safi, huduma bora za afya na barabara za uhakika. Hili ni jambo la aibu kubwa,” amesisitiza.
Katika sekta ya usafirishaji, Doyo amesema madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa za uendeshaji kutokana na ubovu wa barabara, hali inayosababisha biashara zao kushindwa kuleta faida.
Amesema ni jambo lisilo sahihi kwa serikali kudai kodi kubwa kutoka kwa wafanyabiashara hao bila kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu ya barabara unafanyika, jambo ambalo lingesaidia kurahisisha biashara na ukusanyaji wa mapato.
Doyo amesisitiza kuwa CCM imeshindwa kwa miongo kadhaa kutatua changamoto hizo, na sasa wanarudi tena kwa wananchi kuomba kura kwa hoja zilezile ambazo hawajawahi kuzitekeleza.
Miongoni mwa changamoto alizozitaja kuwa kero kwa wananchi wa Sengerema na Buseresere mkoani Geita ni pamoja na ubovu wa barabara, gharama kubwa za usafiri, upungufu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya, ukosefu wa maji safi na salama, pamoja na wakulima kushindwa kupata masoko yenye tija kwa mazao yao.
Baada ya mkutano huo, msafara wa Doyo umeelekea mkoani Kagera, wilaya ya Ngara, kuendelea na kampeni zake kwa wananchi wa maeneo hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED