Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema huduma za Water Taxi zimeanza rasmi visiwani Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kuboresha usafiri wa baharini, kuvutia watalii na kuongeza ajira kwa wananchi.
Akizungumza alipowasili katika Bustani ya African House, eneo lililopatiwa mwekezaji kwa ajili ya uwekezaji wa kisasa wa kitalii, Dk. Mwinyi alisema huduma hizo tayari zimeanza kutoa safari na usafirishaji wa watalii, huku jeti mpya ikiwa njiani.
“Huduma za Water Taxi zimeanza Zanzibar. Hii ni njia ya kisasa ya usafiri wa baharini, itakayochangia kuimarisha utalii na kutoa ajira nyingi zaidi kwa vijana wetu,” amesema Dk. Mwinyi.
Ameongeza kuwa serikali pia inatarajia kuweka miundombinu maalum ya umeme kwa ajili ya kuendesha huduma hizo, ili kuendana na kasi ya dunia katika matumizi ya nishati safi.
Aidha, Dk. Mwinyi amebainisha kuwa mazungumzo ya mradi wa reli ya kisasa kutoka Malindi hadi Bububu tayari yameanza, na muda si mrefu wananchi wa Zanzibar wataanza kunufaika na usafiri huo.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, miradi ya Water Taxi, jeti na reli ni sehemu ya mageuzi makubwa ya sekta ya usafiri Zanzibar, hatua inayothibitisha kuwa visiwa hivyo vinaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo na kujiweka katika ramani ya dunia ya kisasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED