Tanzania ya tatu Afrika mpango rasmi kudhibiti kichaa cha mbwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:44 PM Sep 29 2025
Serikali yazindua mpango kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030
Picha: Mpigapicha Wetu
Serikali yazindua mpango kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa afya ya wanyama imeandaa mpango rasmi wa kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ikiwa ni moja ya mkakati wa kufikia azma ya Dunia ya kuondokana kabisa na ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Agnes Meena katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa yaliyofanyika leo Septemba 29, 2025 Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.

Meena amesema mpango huo ambao umeshapitiwa na kuridhiwa na Shirika la Afya ya Wanyama duniani (WOAH) utaratibu uchanji wa mbwa na paka wote nchini kwa muda wa miaka mitano.

“Kupitia mpango huo, ni imani yetu kwamba hadi kufikia mwaka 2030 Tanzania itakua ni miongoni mwa nchi zitakazokuwa zimeutokomeza ugonjwa huu wa Kichaa cha Mbwa”,amesema Meena.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa wataalam wa mifugo walio karibu yao au serikali ya mtaa ya eneo husika endapo watakutana na mnyama au mfugo wenye dalili zisizo za kawaida.

“Kwa hiyo lengo la maadhimisho haya ambayo yamesababisha tukusanyike hapa leo ni kukumbushana na kuelimishana zaidi jinsi ya kukabiliana na janga hili la ugonjwa wa kichaa cha mbwa”, amesema Meena.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Wanyama wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Benezeth Lutege amebainisha kuwa takwimu zinaonesha mpaka kufikia Septemba 29, 2025 wilayani humo wametoa chanjo kwa Mbwa 3653, Paka 212, Kuhasi Mbwa 96, Paka 5 na Kufunga Vizazi  Mbwa 52, Paka 26. 

Akisoma taarifa ya Wilaya, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Mufandii Msaghaa amesema serikali ya Wilaya hiyo imekuwa ikitekeleza utoaji wa chanjo kwa mifugo na wanyama kwa lengo la kuikinga shidi ya magonjwa na kwamba mchakato huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za mifugo hapa chini.

Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa kwa mwaka 2025 yameenda sambamba na kaulimbiu  isemayo Kichaa cha Mbwa; “Chukua Hatua Sasa, Mimi, Wewe na Jamii.”